Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD yasaidia wanawake wa kisiwani Sumar Ufilipino kujikomboa kiuchumi 

Wakulima wa mpunga wakichukua miche kwa ajili ya kupanda huko Nueva Vizcaya, Ufilipino.
© ILO/Joaquin Bobot Go
Wakulima wa mpunga wakichukua miche kwa ajili ya kupanda huko Nueva Vizcaya, Ufilipino.

IFAD yasaidia wanawake wa kisiwani Sumar Ufilipino kujikomboa kiuchumi 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mradi wa samaki unaofadhiliwa na Mfuko wa  Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo duniani FAO na Serikali ya Ufilipino, umekuwa mkombozi kwa wakina mama ambao hapo awali walikuwa hawana shughuli ya kuwaingizia kipato na sasa wanawake hao, wamejiinua kiuchumi kwa kutumia mbinu walizojifunza enzi za utotoni pamoja na utaalamu wa kisasa waliopatiwa.

Taarifa iliyoandaliwa hapa studio inasomwa kwako na  Happiness Pallangyo wa Radio washirika Radio Uhai FM ya Tabora Tanzania.

Asubuhi ya kupendeza yenye pilika pilika kwa wafanyabiashara wa soko la Guiyang nchini Ufilipino, katika kisiwa cha Sumar kilichoko mashariki mwa nchi hiyo.

Ruperta Gagarin akiuza samaki aliowakausha kwa bei nzuri ya kumpatia faida, lakini hali haikuwa hivi hapo awali anasema, “Sasa naweza kununua chakula, nguo za watoto wangu na vifaa vya shule. Lakini hapo awali hali haikuwa hivi, nilikuwa napata msongo wa mawazo, nilikuwa tu mama wa nyumbani, haikuwa rahisi, kuwanunulia wanangu maziwa ilikuwa kitu kigumu, nilijihisi mnyonge sababu sikuweza kumsaidia mume wangu. Akiwa hana kitu chochote maana yake siwezi hata kuwanunlia watoto maziwa au chakula chetu.“

Ruperta alijifunza kukausha samaki akiwa na umri wa miaka 13 lakini ni miaka michache tu iliyopita ndio aliamua kuubadili utaalamu wake huu kuwa biashara na kuweza kupata faida.

Mradi wa samaki wa kwenye matumbawe unaofadhiliwa na IFAD na serikali ya Ufilipino, umewapatia mafunzo Ruperta na wanawake wengine namna ya kuongeza kipato kwenye samaki wao. Anasema, “kipindi cha nyuma tulikuwa tunajua tuu kupaa samaki, kuwaweka chumvi na kuwaanika, lakini sasa tunatumia teknolojia bora na njia nzuri zaidi za kutengeneza bidhaa zenye ubora. Mradi wa Samaki wa Matumbawe umetupa vikaushio vya kutumia umeme wa jua, meza za chuma kisichoingia kutu, mizani ya kupimia, visu, ubao wa kukatia samaki na mabox ambayo ndio tunaweka bidhaa zetu na kisha tunatoa upepo nakuzifunga , na pia wametupa share zetu tunazovaa. “

Na sasa wanawake hawa wanaweza kuzalisha samaki iwe jua au mvua na hii imesaidia kuwa na uhakiki wa kuwa na uzalishaji endelevu usioathiriwa na msimu wa hali ya hewa.

Mradi huu wa IFAD umesaidia kuhamasisha wanawake kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana uzoefu wao na kutumia kwa pamoja rasilimali chache walizonazo na Ruperta anasema wanafuraha wakati wote hata wakiwa na changamoto.

Wanakikundi hawa wa Taytay wamepatiwa mafunzo ya kutafuta masoko na huduma kwa wateja na sasa wanauza bidhaa zao kwenye maonesho ya biashara pamoja na masoko ya maeneo wanayoishi. “Kwa usaidizi wote tuliopata, kwakweli sasa tuna maendeleo makubwa, hapo awali wanawake wote hawa walikaa nyumbani wakisubiri kuletewa na waume zao, lakini sasa tumeelimika na kuwezeshwa kujitegemea. Sisi wanawake tuna uwezo wetu, uimara wetu na mawazo yetu, hata kwenye kuuza na kufanya mipango mingine yakujipatia fedha, tuifanyie kazi.”

Hivi sasa Ruperta na wanakikundi wenzake wana mipango mikubwa ya kuuza samaki wao katika mikoa mingine na kuwahamasisha wanawake wengine kufuata nyayo zao.