Dunia imekosa mshikamano- Guterres
Dunia imekosa mshikamano- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amehutubia mkutano wa Jukwaa la uchumi duniani, WEF na kuwaeleza viongozi wa sekta ya biashara wanaoshiriki kuwa kinachokosekana hivi sasa duniani ni mshikamano wa kimataifa.
Ametoa hotuba hiyo kwa njia ya mtandao kutoka New York, Marekani kwa sababu mkutano huo kwa mwaka wa pili mfululizo unafanyika mtandaoni badala ya Davos, Uswisi kutokana na janga la coronavirus">COVID-19.
Guterres amesema mkutano wa mwaka huu unafanyika kukiwa na kivuli cha changamoto kubwa zinazokumba siyo tu uchumi wa dunia bali pia wakazi wake na sayari yenyewe ya dunia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwelekeo wa uchumi iliyotolewa wiki iliyopita, dunia inaibuka kutoka kina kikubwa cha janga la kiuchumi lakini kukwamuka bado hali si shwari na ukwamukaji unafanyika bila uwiano miongoni mwa nchi.
Soko la ajira linakumbwa na changamoto, usambazaji wa bidhaa umekumbwa na mkwamo, mfumuko wa bei unaongezeka na nchi zimenasa kwenye mtego wa madeni.
“Miaka miwili iliyopita imedhihirisha ukweli mchungu- iwapo tutamwacha yeyote nyuma, basi kila mtu atasalia nyuma,” amesema Guterres.
Uwiano katika chanjo
Katibu Mkuu amesihi washiriki katika jukwaa hilo kujikita katika maeneo matatu ambayo amesem ani ya muhimu.
Mosi ni kukabiliana na janga la COVID-19 kwa uwiano na usawa huku akikumbusha kuwa lengo la Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO la kupatia chanjo asilimia 40 ya wakazi katika nchi zote mwishoni mwa mwaka jana wa 2021 na asilimia 70 ifikapo katikati ya mwaka huu bado halijakaribiwa kufikiwa.
Amesema ni aibu kwamba katika nchi zilizoendelea kiwango cha utoaji wa chanjo ni cha juu mara saba zaidi ikilinganishwa na nchi za Afrika.
Kando ya kuijkita na uwiano kwenye chanjo, ametaka nchi zijipange na jinsi ya kukabiliana na janga lingine la magonjwa kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya ufuatiliaji, upimaji na uchukuaji wa hatua. Halikadhalika mamlaka za WHO lazima ziimarishwe.
Ametaja jambo la pili kuwa ni hatua za dharura kwa mfumo wa fedha duniani akisema “tunahitaji kurekebisha muundo wa mfumo wa fedha duniani ili uwe na manufaa kwa mataifa yote. Kwa nyakati za sasa muhimu tunajiwekea mfumo wa ukwamukaji usio na uwiano.”
Bwana Guterres amefafanua kuwa katika kila dola 10 zinazotengwa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi baada ya COVID-19, dola 8 zinakwenda nchi Tajiri na kwamba nchi masikini ziko katika upande mkubwa wa kutonufaika.
Kwa sasa nchi maskini zinakabiliwa na kiwango kilichovunja rekodi cha mfumuko wa bei, fursa za kujipatia kipato zimesinyaa, bei za vyakula na nishati zimeongezeka na kwamba mfumo wa fedha umeangusha dunia katika kipindi ambacho unahitajika zaidi kuikwamua.
Unahitajika mfumo unaofaa
Guterres amesema mataifa hayo masikini ambayo yamefungwa pingu za madeni na ongezeko la kiwango cha riba hayakidhi masharti ya kusamehewa madeni licha ya ongezeko la umaskini, ukosefu wa ajira na kurudi nyuma kimaendeleo.
“Tunahitaji mfumo wa fedha duniani unaofaa kushughulikia changamoto za sasa. Tunahitaji kurekebisha madeni, na muundo wa utoaji mikopo pamoja na kupanua wigo wa mfumo wa msamaha wa maden ikwa nchi za uchumi wa kati,” amesema Guterres.
Hatua halisi kwa tabianchi
Jambo la tatu la dharura kwa mujibu wa Guterres ni hatua kwa tabianchi katika nchi zinazoendelea.
Hata kama nchi zilizoendelea zitatekeleza ahadi zao za kupunguza utoaji hewa chafuzi ifikapo mwaka 2030, utoaji wa hewa chafuzi duniani bado utasalia ni wa juu ili kuweza kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5.
Katibu Mkuu amesema ongezeko la nyuzi joto 1.2 tayari limeleta madhara makubwa.
Mwaka jana pekee hali ya hewa kupita kiasi imesababisha hasara dola bilioni 120 na watu 10,000 wamekufa.
Mwaka 2020 majanga ya tabianchi yamesababisha watu milioni 30 kukimbia makazi yao, idadi ambayo ni mara tatu zaidi ya wale waliofurushwa kwa vita na ghasia.
“Kurekebisha mwelekeo kunahitaji utashi wa dhati kutoka kwa serikali na sekta ya biashara katika kila nchi ambayo inatoa hewa chafuzi.” Amesema Guterres.
Vipaumbele
Kwa Katibu Mkuu Guterres, kipaumbele cha kwanza ni kuondokana na makaa ya mawe kwa awamu, akisema hakuna tena kujenga mitambo ya makaa ya mawe.
Na katika maeneo hayo matatu Guterres amesema jamii ya kimataifa inahitaji kuungwa mkono, kupata mawazo, fedha na sauti ya jamii ya kibiashara duniani.
Guterres amesema dunia haiwezi kudurusu tena ukosefu wa usawa na haki ambao unaendelea kutumbukiza makumi ya mamilioni ya watu kewnye umaskini, afya dunia na ukosefu wa mahitaji.
“Hatuwezi kuendelea kujenga ukuta kati ya walionacho na wasionacho” ametamatisha Guterres.