Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Camara Mariama Ciré: Mfano wa kuigwa kupitia kwenye kilimo Guinea Conakry 

Katika umri wa miaka 22 tu, Mariama Camara Cire (katikati) ni mwanafunzi, mkulima na pia mwanzilishi wa chama kinachopiga vita unyanyasaji dhidi ya wanawake. Mariama anaungwa mkono na programu ya ITC ambayo ni taasisi tanzu ya Kamati ya Umoja wa Mataifa y
Screenshot/ITC
Katika umri wa miaka 22 tu, Mariama Camara Cire (katikati) ni mwanafunzi, mkulima na pia mwanzilishi wa chama kinachopiga vita unyanyasaji dhidi ya wanawake. Mariama anaungwa mkono na programu ya ITC ambayo ni taasisi tanzu ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara, UNCTAD na shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara duniani WTO. Programu hiyo kwa ajili ya kuwahusisha vijana katika masuala ya kijamii na kiuchumi (INTEGRA) ni mpango unaokuza ujuzi wa kiufundi na utaalamu wa vijana wa Guinea.

Camara Mariama Ciré: Mfano wa kuigwa kupitia kwenye kilimo Guinea Conakry 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

“Habari, naitwa Camara Mariama Ciré kutoka Guinea Conakry…,” ndivyo anavyoanza Mariama Camara Cire kwa kujitambulisha kuwa anatokea Guinea Conakry moja ya nchi za Afrika Magharibi inayopakana na Bahari ya Atlantiki katika upande wake wa Magharibi na kwingine ikipakana na Guinea Bissau, Sierra Leone, Côte d'Ivoire, Senegal na Mali.

Hivi sasa akiwa na umri wa miaka 22 tu, Mariama Camara Cire ni mwanafunzi, mkulima na pia mwanzilishi wa chama kinachopiga vita unyanyasaji dhidi ya wanawake. Mariama anaungwa mkono na programu ya ITC ambayo ni taasisi tanzu ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara, UNCTAD na shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara duniani WTO. Programu hiyo kwa ajili ya kuwahusisha vijana katika masuala ya kijamii na kiuchumi (INTEGRA) ni mpango unaokuza ujuzi wa kiufundi na utaalamu wa vijana wa Guinea.

Soundcloud

 

Mariama anasema alipokuwa mtoto alizoea kumfata mama yake shambani akimsaidia kazi za hapa na pale…anasema alipokua akaanza kutafuta shamba ili naye aweze kuisaidia familia na kumsaidia mama yake.  

“Baba yangu alininunulia pikipiki ili niwe naambatana naye katika mashamba,” anasema Mariama. Baada ya kuambata naye kwa muda, akapata ujasiri wa kuanza kulima mashamba yake mwenyewe. Anasema walikuwa wanasAfasiri kilomita 20 kwenda kumwagilia mashamba hayo.  

Conakry, mji mkuu wa Guinea
World Bank/Dominic Chavez
Conakry, mji mkuu wa Guinea

 

Mariama anasema, “Tulipanda mbogamboga, nyanya chungu, pipilipili na mahindi.”  

Kupitia shughuli zake za shamba mnamo mwaka 2016 akiwa tu mwanafunzi wa darasa la 10 aliweza kuanzisha shirika lisilo la kiserikali analoliita shirikisho la wasichana na wanawake viongozi wa Guinea ili kupigania haki za wasichana na wanawake. 

“Nilifikiria kuwa ni muhimu kubaki na shughuli zote mbili.”  Anaeleza Mariama akimaanisha kilimo na shughuli ya kuwapigania wasichana wadogo na wanawake.  

Anafadhili NGO kutokana na shughuli zake za kilimo na sasa anamiliki kampuni yake inayoitwa Sonna kwa ajili ya Maendeleo Endelevu.  

“Sonna niliipa jina hilo la mama yangu kwa sababu hajawahi kuacha kunisaidia. Ananifahamu na anajua ndoto zangu.” Anaeleza Mariama. 

Ni wazi kwamba anachokifanya Mariama si tu kinainufaisha familia yake, bali kinainufaisha jamii yake kwa ujumla na kidunia anachangia katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. Mathalani lengo namba 1 linalolenga kutokomeza umaskini, namba 2 linalolenga kutokomeza njaa, namba 5 linalopigania usawa wa kijinsia, namba 8 la ukuaji wa uchumi na mengine kadhaa. Umoja wa Mataifa katika muongo huu wa mwisho wa kuelekea mwaka 2030 uliopangwa kwamba kufikia hapo malengo hayo 17 ya dunia yawe yamefikiwa, unawahamasisha watu kote waliko kushiriki kikamilifu kufanikisha lengo kuu ingawa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kwa kiasi fulani umekuwa kigingi cha kupunguza kasi kama anavyosema Mariana kwamba wakati wa Covid-19 wamekumbana na ugumu mwingi. “Kampuni yangu ilikumbana na changamoto nyingi kwa sababu hatukuweza kuuza vyote tulivyovizalisha hata kwenda sokoni ilikuwa vigumu.” Na kwa msingi huo anaeleza kuwa ajira pia zilipungua kwa kuwa katika kampuni yake wanaajiri vijana wengi na wanawake lakini wakati huo hawakuweza kuwa na zaidi ya watu 20. 

Akiwa anatembea katika shamba lake ambalo limesheheni nyanya chungu ambazo zinaonekana zimemea vizuri na zenye afya ya kupendeza, Mariama anasema anataka kufikia lengo la hiki alichokianzisha. Na ndoto zake zitimie. “Hii leo kupitia shughuli zangu na ujasiri wangu nimekuwa mfano wa kuigwa katika jamii yangu.” Anahitimisha Mariama akitabasamu na kumwegemea mama yake begani.