Tsunami Tonga : Katibu Mkuu wa UN azishukuru nchi ambazo zimeanza kutoa usaidizi 

15 Januari 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa sana na taarifa kuwa Tsunami na majivu  vimeathiri nchi ya Tonga, na kwamba tahadhari ya uwezekano wa nchi nyingine kuathirika imetolewa.

Bwana Farhan Haq ambaye ni Naibu wa Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameeleza kupitia taarifa aliyoitoa Jumamosi hii mjini New York, Marekani kuwa  ofisi za Umoja wa Mataifa katika eneo la Pasifiki zinafuatilia kwa karibu hali hiyo na ziko katika hali ya kusubiri kutoa usaidizi ikiombwa na kwamba, “Katibu Mkuu amezishukuru nchi ambazo tayari zimetoa usaidizi wao.” 

Kwa mujibu wa taarifa za Huduma za Kijiolojia za Tonga, volcano kubwa ya chini ya maji ililipuka kabla ya jioni siku ya Ijumaa kwa saa za Tonga na mlipuko huo kupanda juu angani kiasi cha kufikia zaidi ya maili 12 juu ya usawa wa bahari. Wingu la majivu na mvuke lilifika umbali wa maili 150 hivi, tukio likiwa limenaswa katika picha na video za satelaiti ambazo zimesambazwa na mashirika mbalimbali ya hali ya hewa. 

Taarifa zinaeleza kuwa Tsunami hiyo imesababishwa na mlipuko mkubwa wa Volcano uliotokea katika bahari karibu na nchi hizo za visiwa vidogo vidogo vilivyoko katika bahari ya Pacific. Tahadhari imetolewa katika nchi ambazo ziko karibu nae neo hilo ambazo zinaweza kufikiwa na mawimbi yenye nguvu kutokana na msukumo wa volcano baharini. 

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa ni vigumu kufahamu kiwango cha madhara kwa wat una mali zao kwa kuwa mawasiliano yamekatika huko Tonga ingawa picha na video zinazosambaa mitandaoni zimeonesha watu wakikimbilia katika maeneo ya miinuko ili kuepuka kusombwa na maji ambayo yameonekana yakisambaratisha na kusomba vitu katika fukwe. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter