Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Tuko katika mbio dhidi ya wakati kusaidia watu wa Afghanistan' – Katibu Mkuu UN 

Watoto wakitumia joto la kuni ili kujikinga na baridi katika baridi kali la Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Watoto wakitumia joto la kuni ili kujikinga na baridi katika baridi kali la Afghanistan

'Tuko katika mbio dhidi ya wakati kusaidia watu wa Afghanistan' – Katibu Mkuu UN 

Msaada wa Kibinadamu

Akielezea "jinamizi linalotokea nchini Afghanistan", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, hii leo ameonya kwamba ulimwengu uko "katika mbio dhidi ya wakati kusaidia watu wa Afghanistan." 

Siku mbili tu zilizopita, Umoja wa Mataifa umezindua ombi lake kubwa zaidi la kibinadamu kwa nchi moja, linalohitaji zaidi ya dola bilioni 5 mwaka huu ili kuisaidia Afghanistan. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema ukubwa wa ombi hilo, "unaonesha ukubwa wa kukata tamaa. Watoto wanauzwa ili kulisha ndugu zao. Kufunga vituo vya afya vilivyofurika watoto wenye utapiamlo. Watu wakichoma moto mali zao ili kupata joto. Maisha ya watu kote nchini (Afghanistan) yamepotea." 

Hivi sasa, zaidi ya nusu ya wakazi wa Afghanistan wanategemea msaada wa kuokoa maisha. 

Bila juhudi za pamoja kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Bw. Guterres amesema, "takriban kila mwanaume, mwanamke na mtoto nchini Afghanistan anaweza kukabiliwa na umaskini mkubwa." 

'Matokeo ya kushangaza' 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres, kunapokuwa na ufadhili unaofaa, operesheni ya msaada ina uwezo wa kupata, "matokeo mazuri ya kushangaza." 

Mwaka jana 2021, Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu walifikia watu milioni 18 kote nchini, zaidi ya asilimia 60 zaidi ya mwaka uliopita yaani 2020. 

Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa wafanyakazi wa misaada wanawafikia wat una jamii lakini operesheni za misaada ya kibinadamu kama hii inahitaji pesa zaidi na uwezo wa kubadilikabadilika kuendana na hali.  

"Baridi kali na hali ya kuganda kwa vitu katika mazingira ni mchanganyiko hatari kwa watu wa Afghanistan", Bwana Guterres ameonya akiongeza kuw ni muhimu kuondoa vikwazo au sheria zinazozuia pesa kutumika katika kuokoa maisha na badala yake ufadhili wa kimataifa unatakiwa kuruhusiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wa umma na kusaidia taasisi za Afghanistan kufikisha kwa watu huduma za afya, elimu na huduma nyingine muhimu.