Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kama tunataka kupona kiuchumi 2022 lazima tushirikiane: Guterres

Biashara ya mama ntilie ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika kiasi kikubwa kufuatia vizuizi vya COVID-19 kwenye miji mingi nchini Thailand.
UN Women/Ploy Phutpheng
Biashara ya mama ntilie ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika kiasi kikubwa kufuatia vizuizi vya COVID-19 kwenye miji mingi nchini Thailand.

Kama tunataka kupona kiuchumi 2022 lazima tushirikiane: Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Umoja wa Mataifa umesema ikiwa dunia inataka kupona kwa watu na kuimarika kwa uchumi kwa mwaka huu wa 2022, basi sasa ni wakati wa kuziba mapengo yote ya ukosefu wa usawa ndani, na miongoni mwa nchi na kuimarisha ushirikiano kwa kufanya mambo kama familia moja ya kibinadamu.

Kauli hii imekuja baada ya Benki ya Dunia kutangaza mdororo wa uchumi kwa mwaka huu wa 2022 na kutabiri hali kuwa mbaya zaidi mwakani 2023 huku misaada ya kibinadamu kitarajiwa kupungua kwa nchi zinazoendelea na utofauti wa kiuchumi kuongezeka baina ya nchi za kipato cha juu, kati na chachini. 

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akionya kuwa kuongezeka kwa shinikizo la mfumuko wa bei katika nchi nyingi duniani kunaleta hatari zaidi za kuimarika kwa uchumi.

“Katika kipindi hiki dhaifu na kisicho sawa ambacho uchumi unaenda bila uwiano kwenye kujiimarisha kimataifa, utabiri wa ukuaji kiuchumi uliotolewa na Benki ya Dunia unaonesha wito wa kuchukuliwa hatua bora zaidi za sera na fedha zinazolengwa na kuratibiwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa.” Amesema Katibu Mkuu Guterres 

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya Kiuchumi na Matarajio ya Dunia ya Umoja wa Mataifa (WESP) kwa mwaka 2022 miongoni mwa vichocheo vya kuzorota kwa uchumi ni pamoja na changamoto kubwa zinazoletwa na kuibuka aina tofauti ya Virusi vya COVID-19, changamoto zinazoendelea za soko la ajira, changamoto za ugavi na ongezeko la shinikizo la mfumuko wa bei.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Uchumi na Masuala ya Kijamii Liu Zhenmin amesema “Bila ya kuwa na mbinu endelevu na zilizoratibiwa kimataifa ikiwemo upatikanaji wa usawa wa chanjo kwa wote dhidi ya COVID-19, janga hili litaendelea kuweka hatari kubwa kwa urejeshaji wa uchumi wa dunia ambao unajumuisha wote na ambao ni endelevu.”

Mwanamke akifanyakazi kwenye kiwanda cha nguo huko Lao PDR
© ILO/Jean‐Pierre Pellissier
Mwanamke akifanyakazi kwenye kiwanda cha nguo huko Lao PDR

Nchi za kipato cha chini kuathirika maradufu

Afrika, Amerika ya Kusini ,karibea, na Asia Magharibi zinatarajiwa kuona ahueni ya polepole kwenye uchumi  na hali hiii itaathiri kasi ya uundaji wa nafasi za kazi ili kukabiliana na tatizo la ajira.Kutokana na hli hiyo, idadi ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri inakadiriwa kubaki juu ya viwango vya kabla ya janga la COVID-19, huku umaskini ukitarajiwa kuongezeka zaidi katika nchi za kipato cha chini. Barani Afrika, idadi kamili ya watu wanaoishi katika umaskini inakadiriwa kuongezeka hadi 2023.

Hali ya fedha na madeni ni changamoto hasa kwa nchi nyingi za kipato cha chini na zinazoendelea. Mizigo mkubwa wa deni la nje, ukopaji wa ziada uliofanywa wakati wa janga la COVID-19 na kuongezeka kwa gharama za malipo ya deni kumeweka nchi nyingi katika hali mbaya zaidi.

“Mamlaka za fedha katika nchi zilizoendelea zitahitaji kuharakisha na kuratibu upunguzaji wa manunuzi ya mali na kupunguza mizania ili kusaidia kuwepo kwa utulivu wa kifedha. Nchi hizo tajiri zinapaswa kuweka gharama za kulipa deni la umma kuwa chini, kuhakikisha kuna uhimilivu wa deni na kuepuka ujumuishaji wa fedha mapema”, alisisitiza Hamid Rashid ambaye ni Mkuu wa Tawi la Ufuatiliaji Uchumi Ulimwenguni.