DNA za walinda amani wa Afrika Kusini huko DRC zakusanywa kubaini baba za watoto 

11 Januari 2022

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, jeshi la Afrika Kusini limepeleka timu yake kwenye  ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO,ili kuchunguza vijinasaba vya watoto na wanawake waliobakwa na walinda amani ili hatimaye kuthibitisha iwapo watuhumiwa ni walinda amani kutoka Afrika Kusini na kisha watoto hao watambue baba zao na pia kupatiwa malezi. 

Sakata la ukatili wa kingono unaofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kule wanakohudumu, limesababisha Afrika Kusini ambayo nayo ina walinda amani wake huko DR Congo ichukue hatua kuhakikisha siyo tu kitendo hicho kinatokomezwa bali pia watoto wanatambua baba zao sambamba na malezi. 

Kanali Anina Els Mkuu wa kitengo cha sheria katika jeshi la Afrika Kusini, SANDF, anasema, “hivi sasa timu yetu iko hapa kwenye ujumbe wa MONUSCO  kusimamia ukusanyaji wa sampuli za DNA za akina mama na watoto kwa ajili ya kutambua baba halisi wa mtoto na madai ya matunzo  ya mtoto.” 

Mkurugenzi wa Uamuzi wa Kitabibu kutoka jeshi la Afrika Kusini, Brigedia Jenerali D. Tempelhoff anasema “wameanza kazi hiyo tangu mwaka 2017 kukusanya sampuli za vijinasaba kutoka kwa kila mwanaume mlinda amani anayekwenda kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Hii inafanyika kabla hawajaenda na hii inatuwezesha kushughulikia madai yoyote kutoka kwa mama mwenye mtoto DRC ya kwamba kuna baba wa Afrika Kusini, hivyo tunaweza kumpata haraka mtuhumiwa au kuthibitisha kuwa askari wetu hana kosa.” 

Yewande Owadia ambaye ni Mkuu wa Nidhamu MONUSCO anasema hatua hiyo inaimarisha uwajibikaji, “Hii ni njia ambayo wadai na wale wanaohusika kwenye mchakato wanaona kabisa kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimejizatiti kushughulikia madai ya malezi kutoka kwa baba na pia kutokomeza ukatili wa kingono.” 

Kwa Christine Besong ambaye alikuwa mchechemuzi wa haki za manusura wa ukatili wa kingono, mchakato huu uko wazi kwa kuwa manusura wanafahamu matarajio yao na mchakato mzima wa kile kinachofanyika “kwa hiyo inakuwa rahisi kuwaeleza kuwa kuna mtu yuko kwa ajili ya kuwasaidia katika mchakato mzima.” 

Umoja wa Mataifa unatumai kuwa mchakato huu  utaleta suluhu kwa manusura wa ukatili wa kingono na watoto wao. 

Jeshi la Afrika Kusini lina walinda amani wake kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha MONUSCO kinachohudumu mashariki mwa DRC. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter