Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yazindua mpango wa kusaidia wananchi wa Afghanistan

Familia zilizofurushwa zinakabiliwa na baridi kali na upungufu wa chakula mjini Kabul, Afghanistan
© UNHCR / Andrew McConnell
Familia zilizofurushwa zinakabiliwa na baridi kali na upungufu wa chakula mjini Kabul, Afghanistan

UN yazindua mpango wa kusaidia wananchi wa Afghanistan

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa na washirika wake hii leo wamezindua  mpango wa kusaidia watu milioni 28 wenye uhitaji mkubwa wa misaada ya kubinadamu nchini Afghanistan pamoja na nchi nyingine jirani.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Geneva uswisi ambapo Umoja wa Mataifa na mashirika matano yasiyo ya kiserikali wamelenga kuwasaidai wananchi milioni 22 wa Afghanistan pamoja na wa Afghan wengine milioni 5.7 wanaoishi kama wakimbizi katika nchi tano za jirani sambamba na jamii za wazawa zilizo wakaribisha.

Majanga ya kibinadamu yanaendelea kuikabili nchi hiyo ambapo taarifa zinaeleza kuwa nusu ya watu wanakabiliwa na njaa kali, zaidi ya watu milioni 9 wamekimbia makazi yao, mamilioni ya watoto hawaendi shule, ukiukwaji wa haki za kimsingi za wanawake na wasichana, wakulima na wafugaji wanataabika huku kukiwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, na uchumi unazidi kudorora. Na kama hayo hayatoshi makumi ya maelfu ya watoto wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo huku huduma za kimsingi za afya zikiporomoka.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Martin Griffiths akizungumza katika uzinduzi huo amesema, “ujumbe wangu ni wa dharura: msiwafungie mlango watu wa Afghanistan. Mashirika wa kibinadamu yako tayari, na yanafanya kazi, licha ya changamoto. Tusaidie kuongeza na kuzuia kuenea kwa njaa, magonjwa, utapiamlo na hatimaye kifo kwa kuunga mkono mipango ya kibinadamu tunayozindua leo.”

Mpango huo uliozinduliwa unahitaji dola bilioni 4.44, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi cha msaada wa kibinadamu kuwahi kuzinduliwa. Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi anasema,"Jumuiya ya kimataifa lazima ifanye kila iwezalo kuzuia maafa nchini Afghanistan, ambayo sio tu yangeongeza mateso lakini pia yatasababisha watu wengi kuhama katika nchi hiyo na katika eneo lote. Wakati huo huo, lazima pia tuongeze mwitikio kwa haraka katika kuunga mkono wakimbizi na jumuiya ambazo zimewahifadhi kwa vizazi. Mahitaji ya wakimbizi hayawezi kutupiliwa mbali, wala ukarimu wa nchi zinazowahifadhi hauwezi kuchukuliwa kirahisi. Wanahitaji kuungwa mkono na wanauhitaji leo.”

Ikiwa kiwango hicho cha fedha kitapatikana, mashirika ya misaada yanaweza kuimarisha utoaji wa msaada wa kuokoa maisha wa chakula na kilimo, huduma za afya, matibabu ya utapiamlo, makazi ya dharura, upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, ulinzi na elimu ya dharura.