'Endeleeni kuongea', Katibu Mkuu wa UN ahimiza katika ujumbe kwa Jukwaa la Vijana Ulimwenguni 

10 Januari 2022

Ingawa kila mtu ameathiriwa sana na janga la COVID-19, athari kwa vijana imekuwa "ya kusikitisha sana", ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumatatu. 

Katika ujumbe wa video kwa Kongamano la Vijana Ulimwenguni lilianza leo mjini Sharm el Sheikh, Misri, Katibu Mkuu Guterres amewataka vijana washiriki kusaidia kuunda ulimwengu bora baada ya janga, ikiendana na mada ya mkutano huo akisema, "Kujenga maisha bora ya baadaye kunaanza leo. Kwa hivyo, kwa vijana wanaohudhuria kongamano hili endeleeni kubainisha sukuhu na hatua tunazozihitaji ili kupata nafuu.' 

Wito wa mabadiliko 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akieleza uzito wa tatizo la Covid-19 ameeleza kuwa zaidi ya vijana bilioni 1.6 wametatizika elimu yao, huku ukosefu wa ajira katika vyeo vyao ukiongezeka. Vijana pia wameona upatikanaji wa huduma kama vile huduma za afya na ushauri unapungua, wakati wa kipindi cha changamoto kwa afya ya akili.  

Katibu Mkuu anasema pamoja na vijana kupitia changamoto, “wakati huo huo, wamepiga hatua. Barabani, na mtandaoni, wanatoa wito wa mabadiliko - kudai usawa, amani, haki na hatua juu ya mzozo wa hali ya hewa. Wanasaidiana katika ujirani wao na kwenye mitandao ya kijamii. Na kupitia hafla kama hii, wanatoa maoni na suluhisho juu ya jinsi jamii zinaweza kujijenga tena na kuibuka  

Ujumbe kwa viongozi 

Baada ya kuwaasa vijana kuendelea kupaza sauti, Katibu Mkuu pia ametoa ujumbe kwa viongozi na watunga sera waliohudhuria akisema, "unapotarajia kupona, angalia vijana. Vijana ni chanzo cha ajabu cha mawazo na ufumbuzi wa ubunifu. Mahitaji yao lazima yatangulie katika mijadala ya sera na uwekezaji.” 

Bwana Guterres amehitimisha kwamba anatazamia kusikia matokeo ya kongamano hilo, na kufanya kazi na washiriki kuunda mustakabali bora zaidi. 

Kongamano hilo linaendelea hadi Alhamisi na linafanyika likiwa na kaulimbiu ya Turudi Pamoja: Ulimwengu Baada ya COVID-19, ambayo Bwana Guterres anasema ni ukumbusho kwamba hakuna wakati wa kupoteza. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter