Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Furaha ndani ya familia iliwafanya kukaribia kuuawa na genge la wahalifu nchini Honduras

Nchini Mexico
World Bank/Curt Carnemark
Nchini Mexico

Furaha ndani ya familia iliwafanya kukaribia kuuawa na genge la wahalifu nchini Honduras

Wahamiaji na Wakimbizi

Makundi ya wahalifu nchini Honduras yalibadili kabisa maisha ya familia ya Daina na kusababisha kuikimbia nchi hiyo kwenda kuomba hifadhi nchini Mexico. 

Kauli moja ambayo ni maarufu sana mdomoni mwa wakimbizi kutoka kila kona ya dunia ni kuwa hawakutarajia kama wangeweza kuikimbia nchi yao ili kuokoa maisha lakini kufumba na kufumbua walijikuta wakiacha kila kitu na kukimbia kunusuru maisha yao.

Na kauli hiyo ndio hasa kilichoikuta familia hii ya Dania ambaye miaka 4 iliyopita yeye na mumewake pamoja na watoto wao wawili wakiwa sebuleni ghafla wakashituka nyumba yao ikimimiwa risasi na genge la wahalifu.

Akisimulia anasema walilala chini na kuanza kutambaa sakafuni ili waweze kujificha kuoka maisha yao lakini bahati mbaya risasi moja ilimpata mtoto wakiume wa Dania mguuni. 

Waliweza kuwatoroka watu hao waliowashambulia nyumbani kwao na kumkimbiza mtoto huyo hospitali.

“Mara tu tulipofika hospitalini na mtoto wetu, madaktari walimtoa risasi kwenye mguu wake. Na wakati huo huo, nikaona magari yao yakiwasili. Ilibidi nimkimbize mtoto wangu aliyejeruhiwa nje ya hospitali. Kwa sababu nia ya genge lile ilikuwa ni kuua familia nzima. Sikuwahi kufikiria ningeondoka nyumbani kwangu. Kwa sababu hatukuwa matajiri, lakini tulikuwa na maisha mazuri, tuliishi kwa amani.”

Na hapo ndio maisha yao yakabadilika na kuwa wakimbizi. Miaka minne baada ya kutoroka Honduras, familia hiyo iko imara, yenye furaha, na amani nchini Mexico. Watoto wake sasa wanasoma shule. 

"Tunajenga maisha na mustakabali bora wa baadae wa watoto. Furaha yangu ni kuwaona wakiwa na furaha. Hakuna zawadi kubwa kwa mama kuliko kuwaona watoto wake wakiwa na furaha.”

Si watoto pekee walio katika maisha bora kwa sasa, César ambaye ni mume wa Dania naye amepata kazi katika kiwanda cha samani na hapo anajipatia ujira wa kumuwezesha kuihudumia familia yake. 

"Wakati mtu akiwa na ndoto, hamu, mapenzi ya dhati, na matumaini, ninaamini kuwa hakuna kitu kinachoweza kukuzuia. Naishukuru UNHCR, huwa naitaja, kwa sababu imekuwa msaada muhimu kwa familia yetu.”

Uraia wa nchi ya Mexico

Afisa programu mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Mexico Diego Morales anasema furaha na matarajio haya ya wakimbizi kama Dania yamewezekana kutokana na juhudi za miaka kadhaa za kimapinduzi zilizofanywa na shirika hilo kupitia programu maalum inayofuatilia wakimbizi na waomba hifadhi tangu hatua ya mwanzo ya kuomba hifadhi mpaka mwisho kabisa wanapojumuisha kikamilifu katika nchi waliyohifadhiwa. 

Familia ya Dania na wakimbizi wengine takriban 500 kwasasa wanasubiri kufunguliwa upya kwa mchakato wa kupata uraia kwakuwa sheria za nchi hiyo zinaruhusu wakimbizi waliotambuliwa rasmi na kuishi ndani ya nchi hiyo kwa miaka 2 kupata uraia . Mchakato huo ulisitishwa kutokana na janga la COVID-19 lakini Cesar kifikra yeye na familia yake sasa ni raia wa Mexico wanaosubiri tuu kukabidhiwa rasmi udhibitisho

"Timu ya taifa  ya mpira wa miguu inapocheza, mimi hushangilia Mexico. Lengo letu ni kupata uraia. Tukiweza kufikia hilo kutatufurahi sana. Iitakuwa jambo nzuri sana kwetu.”

Kauli yake inaungwa mkono na mkewake Dania

“ Naamini tutakwenda kujivunia wenyewe. Ninajua mwanangu ataniambia: ‘Mama, yaliyotupata huko nyuma yamekwisha. Sasa nina matarajio makubwa ya baadae maishani, naamini siku moja nitamuona mwanangu akiwa na familia yake hapa.”

Mexico ni moja kati ya nchi 24 duniani zinazotekeleza mpango wa kuwahudumia vyema wakimbizi na waomba hifadhi unaolenga kutafuta suluhu na ushirikiano chini ya UNHCR.