Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wahofiwa kufa katika mashambulizi ya kambi za wakimbizi nchini Ethiopia

Mapigano huko Tigray, Afar na Amhara kaskazini mwa Ethiopia, yamesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu.
IFRC
Mapigano huko Tigray, Afar na Amhara kaskazini mwa Ethiopia, yamesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu.

Watoto wahofiwa kufa katika mashambulizi ya kambi za wakimbizi nchini Ethiopia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limeeleza kukasirishwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya anga kwenye kambi za wakimbizi wa ndani na wakimbizi huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore kutoka jijini New York Marekani imesema, mashambulizi yaliyofanyika Januari 5 na 7 mwaka huu wa 2022 yameripotiwa kujeruhi raia wengi, wakiwemo watoto pamoja na wengine kuuawa. 

"Kambi za wakimbizi na makazi ya wakimbizi wa ndani, ikiwa ni pamoja na shule zinazohifadhi watoto na familia za waliokimbia makazi yao na vifaa muhimu vinavyowapatia huduma za kibinadamu, ni vitu vya kiraia. Kukosa kuwaheshimu na kuwalinda kutokana na mashambulizi kunaweza kujumuisha ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.” Amesema Fore.

Ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa mzozo wa Tigray huko Ethiopia, vitendo vya kikatili, ukatili, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki dhidi ya watoto, vinaendelea kufanywa kaskazini kote mwa Ethiopia na pande zote kwenye mzozo huo, imesema taarifa ya mkuu huyo wa UNICEF na kuongeza kuwa.

"UNICEF inasisitiza upya wito wake wa kusitishwa mara moja kwa uhasama. Tunazitaka pande zote katika mzozo huo kuzingatia na kuendeleza dalili za awali za maendeleo ya kumaliza mzozoz huo zilizoonekana wiki kadhaa zilizopita. Tunasisitiza pia kuzingatia haki za binadamu za kimataifa, sheria za kibinadamu na wakimbizi, kuweka mazingira wezeshi ya ufikiaji wa misaada ya kibinadamu na kulinda watoto dhidi ya madhara ya mzozo huo."