Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli ya Guterres kuhusu Ethiopia na Kazakhstan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
UN Photo/Violaine Martin (file)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Kauli ya Guterres kuhusu Ethiopia na Kazakhstan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua ya Ethiopia ya kuaachia kutoka gerezani watu kadhaa waliokuwa wanashikiliwa wakiwemo wapinzani wa kisiasa.

 Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaeleza waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo ya kwamba Guterres pamoja na kukaribisha hatua hiyo, “anatoa wito kwa pande zote kujenga hatua ya msingi ya kuaminiana kwa kukubaliana usitishaji wa uhasama, kusitisha mapigano na kuanzisha mjadala shirikishi wa kitaifa na mchakato wa maridhiano.”

Guterres amesema ataendelea kushirikiana kikamilifu na wadau katika kusaidia Ethiopia kumaliza mapigano na kurejesha amani na utulivu.
  
“Kufuatia mawasiliano yangu ya mwisho na Waziri mkuu Abiy Ahmed, natarajia kuimarika kwa mfumo wa kupeleka misaada ya kibinadamu katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa mwaka mmoja,” amesema Guterres.
  
Katibu Mkuu amezungumzia pia sherehe za Krismasi ya madhehebu ya Othodoksi akisema “natuma salamu zangu za heri kwa wananchi wote wa Ethiopia wanaosherehekea sikukuu hii. Msingi wa sherehe hizi uchangie katika Ethiopia yenye amani na ustawi,” ametamatisha Guterres.

Kazakhstan zingatia kanuni za kimataifa za kibinadamu

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Msemaji wa Umoja wa Mataifa aliulizwa kuhusu mgogoro unaoendelea huko Kazakhstan na iwapo Katibu Mkuu ana kauli yoyote ya kusema wakati huu ambapo kuna ripoti ya kwamba vikosi vya usalama vimeua waandamanaji.

Akijibu swali hilo Bwana Dujarric amesema, “tazama, tunaendelea kufuatialia kwa ukaribu hali ilivyo Kazakhstan na kwa mara nyingine tena tunasihi wote wale wanaohusika kujizuia kufanya ghasia na kutumia njia za amani kutatua hali ya sasa.”

Amesema watu wanapaswa kuandamana kwa amani na zaidi ya yote, “mauaji ya polisi na watu wengine hayakubaliki, sambamba na mauaji ya waandamanaji. Kuna umuhimu wa kila mazingira kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia viwango vya kimataifa huku ukisaka utulivu wa umma.”

Iliripotiwa jana kuwa vikosi vya usalama vya Kazakhstan vimeua makumi kadhaa ya watu. Halikadhalika watu 1,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo tarehe 2 mwezi huu wa Januari.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kazakhstan inasema askari 12 wamekufa tangu kuanza kwa vurugu hizo huku maafisa wa polisi 317 na walinzi wa kitaifa wamejeruhiwa.

Waandamanaji hayo wanapinga ongezeko la bei ya mafuta sambamba na kuipinga serikali ya Rais Kassym-Jomart Tokayev kwa madai ya ongezeko la ukosefu wa usawa.

Mapema jana, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet akizungumzia matumizi ya risasi za moto kwa waandamanaji, alisema “matumizi ya risasi za moto yanapaswa kutumika pale tu ambapo ni mbinu ya mwisho dhidi ya watu mahsusi ili kuepusha tishio kama vile kifo au majeraha makubwa.”


TAGS: Kazakhstan, Maandamano, Amani na Usalama