Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya waandishi wa habari yalipungua mwaka wa 2021 lakini vitisho vya kutisha bado vibebaki - UNESCO

Waandishi wa habari wakifuatilia kuripoti shambulizi la kigaidi nchini Kenya
©UNESCO/ Enos Teche
Waandishi wa habari wakifuatilia kuripoti shambulizi la kigaidi nchini Kenya

Mauaji ya waandishi wa habari yalipungua mwaka wa 2021 lakini vitisho vya kutisha bado vibebaki - UNESCO

Haki za binadamu

Waandishi wa habari 55 waliuawa katika mwaka uliopita, 2021, uchunguzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni, UNESCO umeeleza. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa theluthi mbili ya mauaji hayo yalifanyika katika nchi ambazo hazikukumbwa na migogoro ya silaha, ikionesha hatari zinazoendelea wanazokabiliana nazo waandishi wa habari katika ripoti zao za kila siku kufichua makosa. 

Hii inaashiria kurejea nyuma kwa hali hiyo miaka michache tu iliyopita, mwaka 2013, wakati thuluthi mbili ya mauaji yalifanyika katika nchi zenye migogoro. 

Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO anasema, "kwa mara nyingine tena mwaka wa 2021, wanahabari wengi sana walilipa gharama kubwa ili kudhihirisha ukweli. Hivi sasa, ulimwengu unahitaji habari huru, za ukweli zaidi kuliko hapo awali. Ni lazima tufanye mengi zaidi ili kuhakikisha kwamba wale wanaofanya kazi bila kuchoka kufanikisha hilo wanaweza kufanya hivyo bila woga.” 

Maeneo mawili hasa ndio yaliyoathiriwa  

Idadi kubwa ya vifo katika mwaka huo wa 2021 ilifanyika katika maeneo  miwili tu ya ulimwengu ambayo ni Asia-Pacific mauaji 23, na Amerika ya Kusini na Karibea, vifo 14. 

“Ikiwa idadi ya mauaji ya waandishi wa habari iko chini zaidi katika kipindi cha muongo mmoja, kutokuadhibiwa kwa uhalifu huu bado kunaenea kwa njia ya kutisha.” Umeeleza utafiti wa UNESCO ukisema kuwa takwimu za UNESCO zinaonesha asilimia 87 ya mauaji yote ya waandishi wa habari tangu 2006 bado hayajatatuliwa. 

Aina mbalimbali za vurugu  

Waandishi wa habari duniani kote pia wanaendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya kufungwa, kushambuliwa kimwili, vitisho na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na wakati wa kufuatilia maandamano. UNESCO inaeleza. 

“Waandishi wa habari wanawake wanakabiliwa hasa na kuenea kwa kutisha kwa unyanyasaji mtandaoni.” UNESCO inafafanua pia ikieleza kuwa ripoti iliyotolewa na UNESCO mwezi Aprili ilionesha karibu robo tatu ya waandishi wa habari wanawake waliohojiwa walikumbwa na unyanyasaji mtandaoni unaohusishwa na kazi zao. 

UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kimataifa la kuhakikisha uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari duniani kote na kuratibu Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Wanahabari na Suala la Kutokuwajibishwa kwa wanaofanya uhalifu, mpango ambao unatimiza miaka 10 mwaka huu wa 2022.  

Shirika hili linalaani kila mauaji ya mwandishi wa habari na kutoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi kamili, kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari na watendaji wa mahakama, kufanya kazi na serikali kuandaa sera na sheria zinazounga mkono, na kuongeza uelewa wa kimataifa kupitia matukio kama vile Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayoadhimishwa. kila mwaka tarehe 3 mwezi Mei.