Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO Yalaani mauaji ya mwandishi wa habari nchini Myanmar

Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.
Unsplash/Alexander Schimmeck
Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.

UNESCO Yalaani mauaji ya mwandishi wa habari nchini Myanmar

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, limelaani mauaji ya mwandishi wa habari Sai Win Aung, anayejulikana pia kama A Sai K, nchini Myanmar yaliyotokea Desemba 25, 2021 nchini Myanmar, karibu na mpaka na Thailand.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari akiwa nchini Ufaransa, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amelaani mauaji ya mwandishi huyo na kutoa wito kwa mamlaka za nchi hiyo kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha mwanahabari huyo.

"Wanahabari kama Sai Win Aung wanahatarisha maisha yao ili kuelimisha umma. Kazi yao inastahili kutambuliwa na usalama wao kuhakikishwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ambayo inakataza mashambulizi yoyote dhidi ya raia. "

Sai Win Aung ni mwanahabari wa pili kuuawa Disemba 2021 nchini Myanmar.

Taarifa hiyo ya mkurugenzi wa UNESCO imeeleza kuwa Sai Win Aung alikuwa anaangazia masaibu ya wakimbizi katika jimbo la kusini-mashariki la Kayin akiandikia jarida la Federal News Journal alipoangushwa na shambulio la mizinga na wanajeshi wa Marekani Myanmar. 

UNESCO inakuza usalama wa waandishi wa habari kupitia kampeni za uhamasishaji za kimataifa, kuwajengea uwezo, na pia kupitia hatua kadhaa, haswa katika mfumo wa Mpango wa Utendaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Wanahabari na suala la kutokujali.