Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha uyoga chakomboa familia nchini Bangladesh

Mamilioni ya watu duniani kote wanategemea misitu kwa ajili ya kipato na chakula
©UNEP/Barbara Schneider
Mamilioni ya watu duniani kote wanategemea misitu kwa ajili ya kipato na chakula

Kilimo cha uyoga chakomboa familia nchini Bangladesh

Ukuaji wa Kiuchumi

Mafunzo ya kilimo cha kisasa cha uyoga na msaada wa kutafutia wakulima masoko ya zao hilo yanayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP yameleta nuru kwa wakulima nchini Bangladeshi akiwemo Sahera Begum ambaye anasema uyoga umemkomboa yeye na familia yake. 

Katika wilaya ya Kurigram Bangladesh uyoga ni zao lenye thamani kubwa sio tu kwa kuwa limesheheni virutubisho vya lishe bali pia kwa kuwakomboa wanawake wengi wilayani hapa waliokuwa mama wa nyumbani wasio na kipato chochote kama Sahera Begum .

Sahera anasema, “uyoga una virutubisho vingi vya lishe na ninapenda kuupika na unaweza kuupika na mboga zingine za majani, Samaki na hata nyama na pia naweza kukaanga vitafunwa kutokana na uyoga.” 

Na hata familia yake sasa wamekuwa wapenzi wakubwa wa kula uyoga sababu ya Sahera akisema, "watoto wangu sasa wanapenda sana kula uyoga na kila mara wananiomba niwakaangie.” 

Sahera baada ya kuwa mke na mama wa nyumbani kwa muda mrefu bila kazi yoyote ya kumuingia kipato alichukua fursa inayotolewa na WFP ya mafunzo ya kilimo cha uyoga kwa ajili ya kuongeza lishe ya familia na kujipatia kipato kwani pia huwatafutia wakulima masoko ya kuuza uyoga wanaovuna. 

Sahera akikumbuka hali ilivyokuwa anasema alichokuwa anafanya ni kazi za nyumbani tu na kusaidia watoto wake kazi zao za shule lakini kwa mafunzo ya WFP sasa zaidi ya hayo analima uyoga. 

Anafafanua akisema, "Uyoga hauchukui nafasi kubwa, nimeshauza kilo 17 na nimekausha kilo 12 na pia nimetumia kilo 5 hadi 7 hivi kwa ajili ya kulisha familia yangu” 

Na skilichosalia kwa Sahera ni kuishukuru sana WFP kwani mbali ya lishe kilimo cha uyoga kimeongeza pato la familia yake na kumpunguzia mumewe mzigo wa kugharamia kila kitu.