Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji wa haki za mtoto duniani umeshamiri- UNICEF

Mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja akiwa na familia yake huko Adra baada ya kukimbia mapigano mji wa Ghouta mashariki mwa Syria
© UNICEF/Omar Sanadiki
Mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja akiwa na familia yake huko Adra baada ya kukimbia mapigano mji wa Ghouta mashariki mwa Syria

Ukiukwaji wa haki za mtoto duniani umeshamiri- UNICEF

Amani na Usalama

Mwaka 2021 ukifikia ukingoni hii leo, shirika la Umoja wa Matafa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema mwaka huu umekuwa wa machungu na ukiukwaji mkubwa wa haki za Watoto katika mizozo ya muda mrefu na ile mipya.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema kuanzia Afghanistan hadi Yemen, Syria hadi kaskazini mwa Ethiopia, maelfu ya Watoto wamekuwa waathirika wakati huu ambapo mizozo ya kivita, mapigano ya kikabila na ukosefu wa usalama vikiendelea kushamiri.

“Wiki iliyopita tu, Watoto wanne waliripotiwa kuwa miongoni mwa watu 35 waliouawa huko jimboni Kayan nchini Myanmar. Hii ni moja ya mifano Dhahiri ya karibuni zaidi ya jinsi mizozo inavyogharimu uhai wa mtoto sambamba na vitisho kwa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu..” imesema taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore akinukuliwa kwenye taarifa hiyo amesema "mwaka hadi mwaka, pande katika mizozo zimeendelea kuonesha kupuuza haki na ustawi wa Watoto. Watoto wanasumbuka, Watoto wanakufa kwa sababu ya ukatili. “Kila juhudi lazima ifanyike ili kuepusha Watoto na majanga.”

Takwimu za mwaka 2021 bado hazijatoka

Taarifa hiyo ikisema kuwa takwimu za mwaka huu mzima zikiwa bado hazijatoka, takwimu za mwak ajana wa 2020 zinaonesha ukikukwaji mkubwa wa haki za Watoto uliothibtishwa na Umoja wa Mataifa.

Miezi ya kwanza ya mwaka 2021 ilishuhudia kupungua kidogo kwa matukio yaliyothibitishwa ya ukatili dhidi ya Watoto lakini matukio 26,425 yaliyothibitishwa ya utekaji, ukatili wa kingono yaliendelea kuongezeka kwa zaid iya asilimia 50 na 10 mtawalia ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka uliotangulia wa 2020.

Maeneo ambako matukio yalithibishwa

Taarifa hiyo inasema matukio ya utekaji nyara Watoto yalithibitishwa kwa kiwango cha juu huko Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, pamoja na nchi za ukanda wa ziwa Chad ambazo ni Chad, Nigeria, Cameroon na Niger.

Kwa upande wake vitendo vilivyothibitishwa vya ukatili wa kingono dhidi ya Watoto vilikuwa vingi zaidi DRC, Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
 
Mwaka huu ni miaka 25 tangu chapisho muhimu la ripoti ya Graca Machel kuhusu athari za kivita kwa Watoto, chapisho ambalo linataka jamii ya kimataifa ichukue hatua thabiti kulinda Watoto dhidi ya vita na pia kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuchukua hatua kulinda Watoto.

Akitamatisha taarifa hiyo ya leo, Bi. Fore amesema “hatimaye Watoto wanaoishi kwenye mazingira ya kivita watakuwa salama pale tu pande kwenye mzozo zitakapochukua hatua kulinda Watoto na kuacha kufanya vitendo vya ukatili. Tunapofunga mwaka 2021 natoa wito kwa pande zote kwenye mizozo kuacha mashambulizi dhidi ya Watoto, zizingatie haki za Watoto na kusaka suluhu ya kisiasa kumaliza vita.”