Chonde chonde , tunawanusru wakimbizi wa Rohingya waliokwama ndani ya boti Aceh:UNHCR 

29 Disemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetoa wito wa kuruhusiwa haraka iwezekanavyo kutia nanga kwa boti iliyosheheni wakimbizi wa Rohingya huko pwani ya Bireuen jimboni Aceh nchini Indonesia, boti ambayo yaelezwa haina viwango na inaweza kuzama wakati wowote huku abiria wengi wakiwa ni wanawake na watoto.  

Boti hiyo kwa mara ya kwanza ilionekana kwenye eneo hilo tarehe 26 mwezi huu wa Desemba.

 Boti hiyo ambayo inasemekana kuwa inavuja na ina injini iliyoharibika, inaelea baharini katikati ya hali mbaya ya hewa na inaweza kuwa katika hatari ya kupinduka na kuzama.

Kwa mujibu wa UNHCR hofu yake kubwa ni usalama na maisha ya wakimbizi waoko ndani ya boti hiyo na kusisitiza kwamba “Ili kuzuia kupotea kwa maisha ya watu, tunatoa wito kwa serikali ya Indonesia kuruhusu mara moja boti hiyo kutia nanga kwa usalama.” 

Kanuni ya Rais ya mwaka 2016 nambari 125 kuhusu ulinzi wa wakimbizi inajumuisha masharti kwa serikali ya Indonesia kuwaokoa wakimbizi kwenye boti walio katika dhiki karibu na Indonesia na kuwasaidia kushuka kwa usalama. 

Masharti hayo yalitekelezwa hapo awali mwaka 2018, 2020 na hivi karibuni mwezi Juni mwaka huu wa 2021, wakati wakimbizi 81 wa Rohingya walipookolewa kwenye pwani ya Aceh Mashariki. 

Mfano wa kuigwa 

 Kwa miaka mingi, Indonesia imekuwa mfano kwa nchi nyingine katika ukanda wa Asia katika kutoa ulinzi kwa wakimbizi.  

UNHCR inatarajia kuona moyo huo huo wa kibinadamu tena leo hii huko Aceh. Warohingya wamekabiliwa na ghasia, mateso na kulazimika kuyahama makazi yao kwa miongo kadhaa sasa. 

“Wale wote wanaotafuta ulinzi wa kimataifa lazima waruhusiwe kuwa na bandari salama na kupewa fursa ya kupata taratibu za hifadhi na misaada ya kibinadamu.” Limeongeza shirika hilo la wakimbizi. 

Wafanyakazi wa UNHCR kwa sasa wako katika eneo hilo, wakifanya kazi kwa karibu na mamlaka za mitaa wakiwa tayari kusaidia serikali na jumuiya ya eneo hilo kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa kundi hilo la wakimbizi.  

Limeongeza kuwa “Pia tunaratibu na washirika wa kibinadamu katika kuandaa hatua ambazo zinajumuisha mchakato wa karantini unaoambatana na viwango vya kimataifa na itifaki za afya ya umma kwa ajili ya kuwalinda wakimbizi hao na jamii itakayowapokea.” 

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter