Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2022 tuazimie kujikwamua kutoka majaribuni- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akizungumza na Yeashea Braddock Meneja wa Operesheni katika shule ya sekondari ya Bronx ambako Katibu Mkuu alipata chanjo ya pili ya COVID-19.
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akizungumza na Yeashea Braddock Meneja wa Operesheni katika shule ya sekondari ya Bronx ambako Katibu Mkuu alipata chanjo ya pili ya COVID-19.

Mwaka 2022 tuazimie kujikwamua kutoka majaribuni- Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma salamu za mwaka mpya wa 2022 akitaka dunia iazimie kwa pamoja mwaka huu mpya uwe wa kuondokana na majaribu yanayotarajia kuikumba.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video Guterres ametaja majaribu hayo kuwa ni  ongezeko la umaskini na ukosefu wa usawa, mgao wa chanjo za COVID-19 usio na uwiano, ahadi za tabianchi zenye pengo, ongezeko la mizozo, migawanyiko na taarifa potofu.

Hata hivyo ametanabaisha kuwa, “haya siyo majaribu ya kisera pekee.
Haya ni majaribu ya kimaadili na maisha halisi. Na ni majaribu ambayo ubinadamu unaweza kufaulu iwapo tutaahidi kuufanya 2022 kuwa mwaka wa kujikwamua.”

Tuazimie kujikwamua 2022

Amesema kujikwamua huko ni kutoka kwenye janga kwa kuwa na mipango thabiti ya kumpatia chanjo kila mtu kokote aliko, kujikwamua kwa uchumi wa nchi, kwa mataifa tajiri kusaidia nchi zinazoendelea kifedha, kiuwekezaji na unafuu wa madeni, kujikwamua kutoka kutokuaminiana na mgawanyiko, kwa kusisitiza kuhusu sayansi, taarifa sahihi na mantiki.

Halikadhalika kujikwamua kutoka kwenye mizozo kwa kuchagiza ari ya mazungumzo, kulegeza misimamo na maridhiano na kujikwamua kwa sayari yetu kwa kutimiza ahadi za hatua kwa tabianchi kulingana na udharura wa janga.

Nyakati ngumu ni nyakati za fursa pia

Guterres ameeleza kuwa, “nyakati ngumu, ndizo pia nyakati za fursa kubwa. Ni nyakati za kushikamana na kuwa na majawabu ya pamoja ya kunufaisha watu wote. Na kusonga mbele kwa pamoja tukiwa na matumaini ya kile ambacho familia yetu ya kibinadamu inaweza kufanikisha.”

Katibu Mkuu ametamatisha ujumbe wake wa mwaka mpya akisema, “kwa pamoja hebu tufanye kujikwamua ndio azimio letu la 2022. Kwa ajili ya watu, sayari na ustawi.Nawatakia nyote mwaka mpya wa furaha na amani.”