Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 31 wafa maji wakiwa safarini kuingia barani Ulaya

Makumi ya maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wanaweka rehani maisha yao ili kuweza kufika Ulaya
IOM/Hussein Ben Mosa
Makumi ya maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wanaweka rehani maisha yao ili kuweza kufika Ulaya

Watu 31 wafa maji wakiwa safarini kuingia barani Ulaya

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesikitishwa na vifo vya hivi karibuni vya watu 31 waliokufa maji katika matukio matatu tofauti ya kuzama kwa boti kwenye bahari ya Aegean.

Bahari ya Aegean ni kipande cha rasi iliyojitokeza kutoka bahari ya Mediteranea kati ya bara la Ulaya na Asia.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi inasema matukio hayo ni kati ya tarehe 21 na 24 ya mwezi huu wa Desemba na kwamba hadi sasa idadi ya watu isiyojulikana bado hawafahamiki waliko.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Ugiriki Maria-Clara Martin amesema “zaidi ya watu 160 wameokolewa na walinzi wa pwani ya Ugiriki, kazi iliyofaniyika kwa msaada wa kikosi cha anga na wanamaji wa taifa hilo la Ulaya pamoja na meli binafsi. UNHCR tunapongeza juhudi za wote waliofanikisha kuokolewa kwa watu hao.”

Mwakilishi huyo amesema ni jambo linaloumiza moyo ya kwamba kutokana na kuhaha kusaka usalama na kwa sababu ya ukosefu wa njia salama na za uhakika, wakimbizi na wahamiaji wanalazimika kuweka maisha yao rehani kupitia kwa wasafirishaji haramu wa binadamu.

“Hatua thabiti zinahitajika ili kuzuia wasafirishaji hao haramu wa binadamu na kutokomeza tabia hizo za watu kutumia majanga ya kibinadamu kujinufaisha. Inavunja moyo  kuona majanga yanayoweza kuzuilika kama haya yakirudia mara kwa mara,” amesema Bi. Martin.

Taarifa zinasema tukio la kwamba lilitokea pwani ya kisiwa cha Folegandros tarehe 21 mwezi huu wa Desemba ambapo watu 13 waliokolewa huku miili ya watu watatu ikiopolewa majini.

Mmoja wa manusura aliwaeleza walinzi wa pwani ya Ugiriki kuwa zaidi ya watu 50 walikuwa kwenye boti ambayo iliwasafirisha bila vifaa vya uokozi.

Katika tukio la pili siku hiyo hiyo ni huko kaskazini mwa kisiwa cha Antikythera ambapo watu 11 walikufa maji na 88 waliokolewa.

Halikadhalika katika mkesha wa sikukuu ya Krismas boti iliyokuwa imebeba watu 80 ilizama kando mwa kisiwa cha Paros na kusababisha vito vya wat u17 akiwemo mtoto mchanga.

Manusura 63 walipelekwa kisiwa cha Paros na kupatiwa huduma ikiwemo matibabu, chakula na mavazi.

UNHCR inakadiria kuwa tangu mwezi Januari hadi Novemba mwaka huu, zaidi ya watu 2,500 wamekufa maji au kupotea bahari katika harakati zao za kutaka kuingia barani Ulaya kupitia bahari ya Mediteranea na njia ya majini ya kaskazini-magharibi mwa Afrika.