Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la bomu huko Beni DRC laua watu 8

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN Photo/Sylvain Liechti
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Shambulio la bomu huko Beni DRC laua watu 8

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO  umelaani vikali shambulio lililofanyika siku ya krismasi na kusababisha vifo vya watu wanane.
 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchiin DRC Bintou Keita ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO amelaani kitendo hicho kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo imesema shambulio hilo la bomu lilifanyika kwenye mgahawa mmoja ulioko mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini.
Vyombo vya habari vinaripoti kuwa shambulio hilo lilifanywa na mtu aliyekuwa amejivika bomu na kisha kujilipua.
Timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS ilifika eneo la tukio ili kusaidia uchunguzi.
Kwa upande wake MONUSCO ilituma timu ya kuendesha doria eneo hilo nyakati za usiku sambamba na kutuma vifaa vya matibabu kwenye hospitali ya mjini Beni.