Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani ghasia na uporaji wa mali El Fasher

Kituo cha Umoja wa Mataifa huko El Fasher kaskazini mwa Darfur nchini SUDAN
UNAMID/Adrian Dragnea
Kituo cha Umoja wa Mataifa huko El Fasher kaskazini mwa Darfur nchini SUDAN

UN yalaani ghasia na uporaji wa mali El Fasher

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani kitendo cha uporaji na ghasia katika kilichokuwa kituo cha ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU wa kulinda amani huko Darfur nchini Sudan, UNAMID.

Ripoti zinasema kuwa uporaji huo na ghasia vimefanyika tangu tarehe 24 mwezi huu wa Desemba katika kituo cha zamani cha UNAMID huko El Fasher ambacho  kilikabidhiwa kwa mamlaka za Sudan tarehe 21mwezi huu wa Desemba

Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu imesema “usalama wa watendaji wa UNAMID ambao bado wako kwenye kituo hicho unasalia jambo muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa hivi sasa. Suala la usalama wa kituo hicho ambacho kimekabidhiwa kwa mamlaka za Sudan unapaswa kuwa chini ya mamlaka za Sudan.”

Umoja wa Mataifa umesema tukio hili la hivi karibuni la uporaji na uharibifu wa mali ni janga kwa jamii za wasudan ambao wanategemea kunufaika na misaada kutoka Umoja  wa Mataifa.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema unatumai kuwa mamlaka za Sudan zitadhibiti uporaji huo huko El Fasher na kwamba miundombinu na vifaa vingine vilivyosalia vinaweza kutumika kwa maslahi ya raia kama ilivyopangwa.

UNAMID ilikamilisha kazi tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2020 na kupisha ujumbe wa pamoja Umoja wa Mataifa wa kusaidia mabadiliko nchini Sudan (UNITAMS) kwa kipidi cha miezi 12 ya kwanza ili kusaidia mchakato wa nchi kuhama kuelekea katika utawala wa kidemokrasia na kuunga mkono ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu na amani endelevu.