Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo cha Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini akimwelezea kuwa “mtu aliyepaza sauti za wasio na sauti bila uoga wowote.”
Kifo cha Askofu Tutu aliyekuwa na umri wa miaka 90 kimetangazwa leo na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jijini New York nchini Marekani imemnukuu Katibu Mkuu akisema “Askofu Desmond tutu alikuwa mnara wa amani duniani na mtoa hamasa kwa vizazi tofauti duniani kote. Wakati wa kipindi kigumu cha ubaguzi wa rangi, alikuwa nguzo ya nuru ya haki, uhuru na kusaka haki bila ghasia.”
Guterres amesema azma ya Askofu Tutu ya kujenga mshikamano wa dunia kwa ajili ya Afrika Kusini huru ilitambuliwa vyema na Kamati ya utoaji wa tuzo za Nobela mbapo mwaka 1984 ilimtunuku tuzo ya amani ya Nobel.
Akiwa mwenyekiti wa Kamisheni ya ukweli na maridhiano Afrika Kusini, Askofu Tutu alitoa mchango mkubwa wa kuhakikisha kipindi cha amani na cha haki cha mpito wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini.
Guterres amesema busara zake na uzoefu mkubwa aliokuwa nao kila wakati alivitumia kuwasilisha joha zake kwa utu, uchezi na moyo wa dhati.
Askofu Tutu alisongesha ushirikiano wa kimataifa
Akizungumzia mchango wake katika ushirikiano wa kimataifa, Guterres amesema Askofu Tutu alikuwa mchechemuzi wa ushirikiaon wa kimataifa na alikuwa na dhima muhimu akitolea mfano mchango wake kama mjumbe wa kipekee wa Kamati ya ushauri ya Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari na katika ujumbe wa ngazi y ajuu wa kusaka ukweli huko Ukanda wa Gaza mwaka 2008.
Katika miongo ya hivi karibuni, Askofu tutu aliendelea kupigania kwa dhati kuchukuliwa kwa hatua kwenye masuala kadhaa kama vile umaskini, mabadiliko ya tabianchi, Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi.
Katibu Mkuu amesema “ingawa kifo cha Askofu Tutu kinaacha pengo kubwa kimataifa na katika nyoyo zetu, daima tutahamasika na mfano wake kuendeleza mapambano ya kuhakikisha dunia inakuwa pahala bora kwa kila mtu.”