Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka ukimbizi arejea nyumbani na kufuga kuku sasa ni mfano kwa wenzake Burundi

Daktari wa mifugo akimchunguza kuku mgonjwa.
FAO/Giulio Napolitano
Daktari wa mifugo akimchunguza kuku mgonjwa.

Kutoka ukimbizi arejea nyumbani na kufuga kuku sasa ni mfano kwa wenzake Burundi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kijana Evariste Niyonzima mkazi wa sasa wa viunga vya jiji la Bujumbura nchini Burundi aliporejea nchini mwake kutoka ukimbizini katika nchi jirani ya Tanzania, alikuwa na mawazo kuwa atakapomaliza tu masomo atapata ajira ya ofisini itakayompa kipato hadi pale alipogundua kuwa hali halisi ni tofauti na alivyofikiria. Hata hivyo hivi sasa amefanikiwa kuliko hata baadhi walioajiriwa ofisini. Alifanyaje? Edwije EMERUSENGE ni mwandishi wa Televisheni washirika, Mashariki TV ya Burundi ameipata siri ya mafaniko anasimulia zaidi.

Baada ya kijana Evariste Niyonzima kurejea kutoka ukimbizi alijiendeleza kwa masomo ya elimu ya juu hadi chuo kikuu. Hali ya upatikanaji wa zinazoitwa ajira rasmi  ilipokuwa tete akaamua kuanzisha mradi wa ufugaji ambao alianza na kuku hamsini.

“Ninajivunia huu ufugaji kwa sababu unanifanya niishi. Hapa kila kitu ambacho unakikuta hapa cha gharama kinalipwa na huu ufugaji wa kuku. Kwa hivyo ninajivunia ufugaji huu kwa kuwaunanitunzana unaitunza familia yangu.” Anaeleza Evariste akiongeza kusema, “faida nyingine ni kwamba ninazalisha vifaranga. Wapo watu ambao wanakuja kununua na wakinunua wanaenda na wao wanapata mayai, wanapata nyama ndio naweza kujivua hata hilo pia kwa sababu sio mimi pekee. Watu wengi wakipata kuku maana yake uchumi unapanda.”

Kama ilivyo miradi mingine yoyote, ufugaji wa kuku nao una changamoto zake, lakini Evariste anasema kilichomsaidia ni kuzingatia tu mawazo chanya kama anavyoeleza, “mara ya kwanza kuingia katika mradi, kuna matishio kwamba mradi unaweza kukwama. Kuna upande chanya na upande hasi, mimi nimeangalia upande mzuri yaani upande chanya. Kwa sababu ukiangalia kwamba utashindwa, basi unaweza ukashindwa lakini mimi sikuangalia kusindwa, mimi niliangalia kwamba nitaendelea mbele.”