Kimbunga Rai: Idadi ya majeruhi na vifo tuliyonayo inaweza kuongezeka - OCHA  

23 Disemba 2021

Baada ya kuhitimisha ziara yake katika maeneo yaliyoathiriwa, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu nchini Ufilipino, Gustavo Gonzalez, leo Desemba 23 amesema Kimbunga Rai "kimekuwa cha uharibifu," na kubainisha kuwa katika siku zijazo, idadi ya majeruhi na waliofariki "bila shaka" itaongezeka.

Wakati wa ziara yake, Gonzalez amesema, ameona, "barabara zilizofunikwa na vifusi, mitandao ya umeme ikiwa chini, mamia ya nyumba bila paa, na bila shaka athari kwa watu."

Bwana Gonzales amesema, “unaweza kuona watu kandoni mwa ukingo wa barabara kati ya Butuan na Surigao wakiomba, wakiomba msaada sana. Na wanaomba hifadhi ya dharura, maji ya kunywa, chakula, na ustawi wao.”

Aidha kiongozi huyo amebainisha kuwa, "kinyume na utabiri, Kimbunga Rai kiliongezeka kutoka kwa dhoruba ya kitropiki hadi kimbunga kikali ndani ya saa chache."

"sote tulishangaa kimbunga hiki kilitokea katika eneo ambalo halikutarajiwa, sio eneo la jadi ambalo tuna mwelekeo wa vimbunga, na jinsi kilivyoibuka kwa njia fulani viliathiri hatua zetu za kutarajia." Amesema.

Watu milioni tatu wanahitaji msaada, ikiwa ni pamoja na "takribani watoto milioni moja," Gonzalez almeeleza, akiongeza kuwa "takribani watu 177" wamefariki dunia, wakati 275 wamejeruhiwa. Watu 650,000 wamesalia bila makazi.

Vile vile Bwana Gonzales amesema, "tunakabiliwa na hali ambayo hatuwezi kufikia visiwa, hatuwezi kuwasiliana na mamlaka za maeneo. Kwa hiyo, hatushangai labda siku zijazo takwimu tunazotumia zitabadilika na hakika zitaongezeka.”

Covid-19 nayo

Afisa huyo ameonesha wasiwasi wake kuhusu kukatizwa kwa kampeni ya chanjo ya COVID-19 katika eneo lililoathiriwa akisema, "ukweli kwamba hakuna umeme, hii inaathiri minyororo wa baridi ya uhifadhi wa chanjo, na wakati huo huo maabara, na katika uhamishaji, ni vigumu kuhakikisha kuheshimu nafasi kat ya mt una mtu na matumizi ya barakoa."

Kimbunga Rai, kinachojulikana kama Kimbunga Odette nchini Ufilipino, kilitua tarehe 16 mwezi huu wa Desemba kikiwa na pepo zenye kasi ya kilomita 195 kwa saa (maili 121 kwa saa), na upepo mkali wa hadi 270kph (168 mph) katika mikoa ya kisiwa cha kati cha Ufilipino.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter