Uchaguzi wa haki 2022 Lebanon, utakuwa "fursa muhimu" kwa wananchi kusikika - Guterres 

21 Disemba 2021

Baada ya kusikiliza na kuona kwa macho yake mateso ya watu wa Lebanon, hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaambia viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kwamba "hawana haki ya kugawanywa", na kuliacha taifa likiwa limepooza, katikati ya migogoro mingi.

“Taasisi zote za Serikali zinapimwa kwa matokeo: ulinzi wa jamii, upatikanaji wa umeme na maji, elimu na huduma za msingi za afya, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu.” Amesema Bwana Guterres. 

Jukumu muhimu 

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuashiria mwisho wa ziara yake ya siku tatu ya mshikamano, amesema kuwa ikiwa nchi itarejea tena katika njia ya kupona, "mashirika ya kiraia, wanawake na vijana wana jukumu muhimu la kutekeleza" na kwa hivyo, "Sauti zao lazima zisikilizwe, na mapendekezo yao yazingatiwe kwa umakini. Uchaguzi huru na wa haki wa wabunge, ulioandaliwa kwa mwaka 2022, utakuwa fursa muhimu kwa wananchi kutoa sauti zao.” 

Aidha Bwana Guterres amesema anashukuru kwa kuweza kukutana na kuzungumza  na jamii mbalimbali za Lebanon, zikiwemo mamlaka za kisiasa na kijeshi, pamoja na viongozi wa kidini. 

Pia amefanya ziara kaskazini na kusini mwa nchi na kuwaambia waandishi wa habari imekuwa "heshima" kurudi katika nchi anayoipenda sana. 

“Lakini inanihuzunisha sana kuona watu wa nchi hii nzuri wakiteseka sana. Watu wa Lebanon wanakabiliwa na changamoto kubwa,” amesema Guterree akiongeza kwa kusema, "hata hivyo licha ya shida wanazovumilia, joto na ukarimu wa watu wa Lebanon unaendelea kung'aa."  

Katibu Mkuu Guterres amesema ukanda na dunia nzima wanashukuru kwa ukarimu wa nchi hiyo katika kuwapa hifadhi Wasyria na wengine wanaokimbia migogoro mikali na kupongeza "roho ya kuishi pamoja na kuvumiliana" kutoka kwa nchi hiyo iliyoko Mashariki ya kati. 

Waathiriwa Wanastahili Majibu 

Kuhusu mlipuko katika Bandari ya Beirut, ambapo zaidi ya watu 200 walifariki dunia katika milipuko mikubwa ya Agosti 2020, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amerejelea maoni yake kwamba "waathiriwa wote wanastahili majibu na haki ambayo haiwezi kutolewa tu pasi na uchunguzi usio na upendeleo, wa kina na wa uwazi ”. 

Kuhusu uchumi wa wananchi, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya athari za mzozo wa kiuchumi na kifedha unaozidi kuwa mbaya ambao umechochewa na mkwamo wa kisiasa, udini, maandamano makubwa na hali ya dharura ya kibinadamu inayoongezeka. 

"Jana nilitembelea Tripoli kaskazini mwa Lebanon na leo Tire kusini mwa nchi. Nimeguswa sana niliposikiliza maelezo ya moja kwa moja ya athari za janga hili katika maisha ya kila siku ya watu." Amesema Bwana Guterres. 

Wasikilizeni watu 

"Watu wanatarajia viongozi wao wa kisiasa kusikiliza mahitaji yao na kurejesha uchumi, ikiwa ni pamoja na kupitia serikali na taasisi za serikali, na kwa kushughulikia rushwa ipasavyo. Kwa siku mbili zilizopita, nimewahimiza viongozi wa kisiasa wa Lebanon kufanya kazi katika kutekeleza mageuzi ambayo yanakidhi matakwa ya watu wa Lebanon kwa ustawi zaidi, uwajibikaji, ulinzi na uwazi, ili kurejesha matumaini ya maisha bora ya baadaye ". Bwana Guterres ameshauri na kusisitiza. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter