Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wameikimbia Cameroon kuingia Chad, hali ni tete - UNHCR 

Wakimbizi kutoka Cameroon baada tu ya kuwasili katika mkoa wa Chari Baguirmi nchini Chad karibu na mji mkuu N’Djamena.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Wakimbizi kutoka Cameroon baada tu ya kuwasili katika mkoa wa Chari Baguirmi nchini Chad karibu na mji mkuu N’Djamena.

Maelfu wameikimbia Cameroon kuingia Chad, hali ni tete - UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema mapigano kati ya jamii yaliyozuka katika eneo la Kaskazini nchini Cameroon katika wiki mbili zilizopita yamewafurusha takribani watu 100,000 kutoka katika makazi yao, ingawa idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi. Taarifa ya Jason Nyakundi inaeleza zaidi. 

Katika eneo la Oundouma nchini Chad, ni watoto wa umri wa kuanza shule na hata wale wa chini ya miaka mitano, wanawake na wanaume wazee na hata wajawazito ilimradi kila mmoja amekimbilia hapa kuokoa maisha yake baada ya jamii zao kupigana huko nchini mwao Cameroon. 

Takriban watu 48,000 wamepata hifadhi katika maeneo 18 ya mijini huko N’Djamena, mji mkuu wa Chad, na watu 37,000 wametawanyika katika maeneo 10 ya mashambani kando ya ukingo wa Chad wa Mto Logone asilimia 98 ya watu wazima ni wanawake. UNHCR inakadiria kuwa zaidi ya watu 85,000 wamekimbilia hapa Chad katika siku za hivi karibuni, wakati takriban raia wengine 15,000 wa Cameroon wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Kwa kuwa kuna ugumu wa watoa misaada kufika katika eneo hilo, UNHCR inasema idadi hizi zinaweza kuwa za juu zaidi.  

Mkimbizi mmoja anayefahamika kwa jina Saleh Abderrahmam huku akionesha majeraha makubwa mgongoni na kichwani anasema,“nilijeruhiwa kwa panga kichwani na kwa visu mgongoni. Baada ya siku tatu msituni, niliweza kuvuka Mto Logone hadi kufikia eneo la Oundouma.” 

Hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, UNHCR inasema watu waliouawa katika mapigano hayo kijamii wameongezeka na kufikia 44 na waliojeruhiwa 111. Kwa jumla, vijiji 112 vilichomwa moto. Mkimbizi mwingine, Fane Tahir anaeleza aliyoyashuhudia akisema, “watu sita wa boma langu waliuawa, akiwemo mume wangu na mtoto wangu mmoja. Nyumba yetu iliteketezwa kwa moto baadaye.” 

Kwa kushirikiana na mamlaka za Chad, UNHCR na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wanaharakisha kutoa msaada wa kuokoa maisha. Barnabe Nambatingar ni Afisa wa UNHCR anaeleza kinachoendelea, "tunamvalisha bangili mkononi kila mtu ili tuweze kuwatofautisha na wakazi wa eneo hilo. Tunasambaza vyakula vya moto, kujenga vyoo na tumepeleka kliniki zinazohamishika kwenye maeneo hayo kwa ajili ya huduma ya kwanza.” 

UNHCR inasema wakimbizi wanahitaji sana makazi, blanketi, mikeka na vifaa vya usafi. Baadhi wanahifadhiwa na jamii za wenyeji, lakini wengi wao bado wanalala katika maeneo ya wazi na chini ya miti.