HRC kuanzisha tume ya kimataifa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu Ethiopia

17 Disemba 2021

Wasiwasi mkubwa wa madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukatili mwingine nchini Ethiopia unapaswa kuchunguzwa na chombo cha kimataifa cha haki za binadamu, limeafiki Baraza la Haki za Kibinadamu hii leo kupitia kura maalum. 

Katika kikao maalum kilichofanyika mjini Geneva Uswis kwa ombi la Muungano wa Ulaya, kujadili athari za mzozo ulioanza huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia miezi 13 iliyopita, wajumbe wameambiwa kuwa watu tisa kati ya 10 katika eneo hilo sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu. 

Ili kikao maalum kifanyike, basi thuluthi moja ya wajumbe 47 wa Baraza lazima waunge mkono ombi hilo. 
Hatua hiyo inafuatia kuongezeka kwa mapigano ya hivi majuzi kaskazini mwa Ethiopia ambayo yametishia kuyumbisha nchi nzima na eneo kubwa la Pembe ya Afrika. 

Akihutubia Baraza hilo, Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu Nada Al-Nashif amesema “Kuna uwezekano kwamba zaidi ya watu 400,000 huko Tigray wanaishi katika hali ya njaa, kwani ni msaada mdogo tu ambao umeruhusiwa kuingia katika eneo hilo tangu wati misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa walipotoa tahadhari mwezi Juni.” 

Mtoto mdogo anachunguzwa ukosefu wa lishe bora katika eneo la usambazaji wa chakula huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
© WFP/Claire Nevill
Mtoto mdogo anachunguzwa ukosefu wa lishe bora katika eneo la usambazaji wa chakula huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Wito wa kusitisha mapigano  

Kamishina huyo msaidizi amesema baada ya kuzitaka pande zinazozozana kuheshimu wito wa mara kwa mara wa kimataifa wa kusitisha mapigano, takriban watu milioni mbili katika maeneo ya Tigray, Amhara na Afar wameyakimbia makazi yao kwa sababu ya migogoro na "wengi wao hawapati msaada wanaohitaji ili kuendelea kuishi.” 

Maoni yake yamekuja kabla ya kupigwa kura juu ya rasimu ya azimio mbele ya Baraza ya kuunda tume ya kimataifa ya wataalam wa haki za binadamu nchini Ethiopia, ambayo kura ambayo imeungwa mkono na nchi 21 ambapo 15 zilipinga na 11 zikijizuia kupiga kura. 

Kulingana na azimio hilo, uchunguzi huo mpya unapaswa kujumuisha wataalam watatu wa haki za binadamu, wote walioteuliwa na Rais wa Baraza la Haki za Kibinadamu. 

Kwa kuanzia tume hiyo mpya imepewa muda wa mwaka mmoja lakini iinauwezekano wa kuongezewa muda, na kazi ya uchunguzi huo wa kimataifa itakamilisha kazi ambayo tayari imefanywa na timu ya pamoja ya uchunguzi inayohusisha ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia katika kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, masuala ya kibinadamu na sheria ya wakimbizi ukiukwaji unaotekelezwa na pande zinazohusika katika mzozo wa Tigray. 
Kukamatwa kwa idadi kubwa ya watu 
 
Naibu Mkuu wa Haki za Umoja wa Mataifa amebainisha kwa wasiwasi mkuwa kwamba hali ya hatari ya nchi nzima iliyotangazwa tarehe 2 Novemba imesababisha kukamatwa kwa watu wengi wanaoaminika kukiunga mkono chama cha Tigrayan People's Liberation Front (TPLF). 

Ameongeza kuwa Maelfu ya watu wa kabila la Tigrayan wamezuiliwa, pamoja na waandishi wa habari zaidi ya 12 na wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa pia. 

"Wakati baadhi ya wale waliokamatwa katika muda wa wiki sita zilizopita wameachiliwa, tunakadiria kuwa kati ya watu 5,000 na 7,000 wamesalia kizuizini, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi tisa wa Umoja wa Mataifa. Wengi wanazuiliwa bila mawasiliano au katika maeneo yasiyojulikana. Hii ni sawa na kutoweshwa kwa lazima, na ni jambo la kutisha sana." 

Bi. Al-Nashif pia ameitaka Serikali ya Ethiopia "kutoa mashauri ya haki na huru ambayo yatashughulikia kwa kina ukiukaji uliobainishwa. Bila ya juhudi kubwa za uwajibikaji, utaratibu wa kimataifa unaweza kuwa mchakato muhimu." 

Pia amezihimiza pande zote kushiriki katika mazungumzo yenye tija na jumuishi kupitia Tume ya Kitaifa ya mazungumzo na katika muktadha wa juhudi za upatanishi za Muungano wa Afrika. 

Wakizungumza kama nchi husika, ujumbe wa Serikali ya Ethiopia umepiga shughuli za Baraza hili ukidai ni uingiliaji uliochochewa kisiasa, kabla ya kusisitiza kusisitiza kwake bila kipingamizi kuhusu haki za binadamu.

Kikao maalum cha leo ambacho ni cha tano kwa mwaka huu katika baraza hilo lenye makao yake makuu Geneva hakijashutumu "uporaji, uharibifu wa mali, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, matumizi ya askari watoto vitani na vikosi hivi vya waasi, TPLF", amesema Balozi Zenebe Kebede wa Ethiopia.

Umoja wa Mataifa unatoa dola milioni 20 ili kupunguza upotevu wa maisha na kupungua kwa matumizi ya chakula baada ya mvua kunyesha katika maeneo ya Ethiopia kukosa maji.
FAO/Michael Tewelde
Umoja wa Mataifa unatoa dola milioni 20 ili kupunguza upotevu wa maisha na kupungua kwa matumizi ya chakula baada ya mvua kunyesha katika maeneo ya Ethiopia kukosa maji.

Mbinu za kigaidi 

Akilielezea TPLF kama kundi la kigaidi, balozi Kedebe ameongeza kuwa wapiganaji wa kundi hilo waliamuru "zaidi ya malori 1,000 yaliyokuwa yakipeleka vifaa vya kibinadamu kwa watu katika mkoa wa Tigray kutofanya hivyo na kutumia msaada huo kwa madhumuni ya kijeshi". 

Kundi la Watigray waliojitenga pia walikuwa wameharibu maghala ya chakula, shule, vituo vya afya na bustani za viwandani, lakini "waanzilishi wa Kikao hiki Maalum hawatajali hata kidogo kuhusu hilo", amesisitiza mwakilishi huyo wa Ethiopia. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter