Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Hatuwezi kushinda janga la Covid-19 kwa njia isiyoratibiwa' – Katibu Mkuu wa UN 

Mwanamke akipimwa joto lake kabla ya kuingia katika hospitali ya Bulawayo, Zimbabwe
ILO/KB Mpofu
Mwanamke akipimwa joto lake kabla ya kuingia katika hospitali ya Bulawayo, Zimbabwe

'Hatuwezi kushinda janga la Covid-19 kwa njia isiyoratibiwa' – Katibu Mkuu wa UN 

Afya

Akijenga hoja kwamba ulimwengu "hauwezi kushinda janga kwa njia isiyoratibiwa", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Alhamis amesema kwamba nchi "lazima zichukue hatua madhubuti katika siku zijazo" kuchanja asilimia 40 ya idadi ya watu wote ulimwenguni ifikapo mwisho wa mwaka.  

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao mjini New York, Bwana António Guterres pia ameziomba Nchi Wanachama "kuwa na matamanio zaidi" katika jitihada zao za kufikia asilimia 70 ya watu katika nchi zote ifikapo katikati ya 2022, lengo lililoanzishwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO

Siku chache tu kabla ya tarehe ya mwisho, nchi 98 hazijaweza kufikia lengo hilo la mwisho wa mwaka, na mataifa 40 bado hayajaweza hata kuchanja asilimia 10 ya watu wao. Katika nchi zenye kipato cha chini, chini ya asilimia 4 ya watu wanapata chanjo. 

Upenyo kwa mnyumbuliko wa Virusi  

"Ukosefu wa usawa wa chanjo unaipa minyumbuliko  njia ya bure ya kukimbia, kuharibu afya ya watu na uchumi katika kila kona ya dunia." Bwana Guterres amesema. 

Kwa mujibu wa WHO, viwango vya chanjo katika nchi zenye mapato ya juu ni mara 8 zaidi kuliko katika nchi za Afrika. Kwa viwango vya sasa, bara hilo halitafikia kiwango cha asilimia 70 hadi Agosti 2024. 

Kwa sababu ya hayo yote, Katibu Mkuu anaamini kwamba "COVID-19 haiondoki." 

"Inazidi kuwa wazi kuwa chanjo pekee hazitamaliza janga hili. Chanjo zinazuia kulazwa hospitalini na kifo kwa wengi wanaozipata na kupunguza kasi ya kuenea. Lakini uuambukizaji hauoneshi dalili ya kuacha. Hii inachochewa na ukosefu wa usawa wa chanjo, kusitasita na kuridhika." 

"Mwaka mgumu" 

Katika mkutano wake huu wa mwisho na waandishi wa habari mwaka huu mjini New York, Bwana Guterres amesema ulimwengu "unakaribia mwisho wa mwaka mgumu". 

Mwaka huu 2021, amesema Guterres, janga bado linaendelea, ukosefu wa usawa umeendelea kuongezeka, mzigo kwa nchi zinazoendelea ulikua mzito na shida ya hali ya hewa imebaki bila kutatuliwa. 

“Nina wasiwasi mkubwa. Ikiwa mambo hayataboreka na kuimarika haraka, tunakabiliwa na nyakati ngumu zaidi mbeleni." Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya.