Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yanusuru watoto wenye utapiamlo Garissa Kenya

wafanyabiashara wa mifugo katika soko la Garissa, Kenya
FAO/Thomas Hug
wafanyabiashara wa mifugo katika soko la Garissa, Kenya

UNICEF yanusuru watoto wenye utapiamlo Garissa Kenya

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaendesha program maalum ya lishe kwenye kaunti ya Garissa nchini Kenya kwa lengo la kunusuru maisha ya mamia ya watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo.

Jason Nyakundi na taarifa zaidi 
(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI) 
Nattsss…. 
Katika kaunti ya Garissa nchini Kenya ukame umetamalaki na kuathiri sio tu mifugo bali wananchi wa eneo hili wakiwemo mamia ya watoto  ambao sasa wana utapiamlo kama anavyosema Shahmat Yusuf mratibu wa lishe katika kaunti hii 
 
(SAUTI YA SHAHMAT YUSUF-MELLISSA) 
“Katika kaunti ya Garissa ukame umetuathiri sana kiasi kwamba tuko katika mgogoro, na vyanzo vyote vya maji vimekauka hivyo hii ndio hali halisi. Watu wengi wamehama kutoka kwenye vijiji vyao na kukimbilia mjini na watoto wengi wameathirika. Katika kila watoto 100, kumi na saba kati yao wana utapiamlo na endapo mvua haitonyesha basi hali itakuwa mbaya zaidi” 
Mmoja wa wazazi Kah Hassan anasema ilimlazimu kukimbia kwenda kuishi na ndugu mjini maana hakuwa na maji wala chakula cha kulisha watoto wake ambao ni wadogo na hakuweza kulipa kodi ya pango. 
Lakini sasa kupitia kampeni na mradi wa lishe wa UNICEF kwa kushirikiana na wizara ya afya ya Kenya na maafisa lishe wa kaunti wanapita nyumba kwa nyumba kupima watoto na kutoa mapendekezo ya kuwasaidia wale wenye utapiamlo kama anavyofanya afisa wa afya ya jamii wa kujitolea Mohammed Omar  ambaye anasema “Nilipomtembelea Kah nyumbani niliwapima watoto wake na nikamshauri awapeleke hospitali kwa sababu walikuwa na utapiamlo.” 
Mbali ya huduma UNICEF inasaidia pia kutoa chakula chenye lishe kwa watoto na mafunzo kwa wahudumu wa afya ya jamii  ili kuweza kukabiliana na changamoto za utapiamlo. 
Mafunzo wanayotoa yamekuwa mkombozi kwani yanawasaidia sana wahudumu wa afya kubaini watoto walio na utapiamlo na kuwapa matibabu yanayostahili lakini pia kwa wazazi imekuwa faraja ya kuwaondolea hofu ya kupoteza watoto wao kwa ugonjwa ambao unatibika. 
TAGS: UNICEF, utapiamlo, Watoto, Garissa, Kenya