Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaanza utoaji chanjo kwa wahamiaji 7,500 waliokwama Yemen

Mhamiaji wa Ethiopia nchini Yemen anapokea chanjo yake ya COVID-19 katika Kituo cha Majibu cha Wahamiaji cha IOM huko Aden.
IOM/Majed Mohammed
Mhamiaji wa Ethiopia nchini Yemen anapokea chanjo yake ya COVID-19 katika Kituo cha Majibu cha Wahamiaji cha IOM huko Aden.

UN yaanza utoaji chanjo kwa wahamiaji 7,500 waliokwama Yemen

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM leo limeanza kampeni ya chanjo ya COVID-19 kwa wahamiaji waliokwama nchini Yemen.  

Lengo ni kuwachanja karibu watu 7,500 katika vituo vyake vya kuhudumia wahamiaji vilivyoko huko Aden na Ma'rib. 

Mkuu wa operesheni za IOM nchini Yemen, Christa Rottensteiner, ameeleza kwamba "kuwachanja watu wanaosafiri ni muhimu katika kupambana na kuenea kwa ugonjwa huo." 

Kwa mujibu wa IOM takriban wahamiaji 36,000 wamekwama katika safari zao kutokana na vikwazo vya uhamaji, na takriban 3,500 huko Ma'rib pekee. Wengi wanalala katika mazingira yenye msongamano na yasiyo safi ambapo virusi vinaweza kuenea kwa urahisi. 

Bi. Rottensteiner  ameongeza kuwa "Kuchanja dhidi ya COVID-19 ni muhimu zaidi katika maeneo kama Ma'rib ambapo migogoro inayoendelea inaendelea kudhoofisha vituo vya afya na kutatiza usambazaji wa dawa.”

Kulingana naye, bado hakuna dozi za kutosha kulinda kila mtu nchini Yemen dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. 

Kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba "Msaada zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa unahitajika ili kuipatia nchi hiyo chanjo ya kutosha itakayookoa maisha,"  

Janga kubwa 

Shirika hilo la wahamiaji linasema kufikia sasa, janga hilo limekuwa na athari mbaya kwa afya, ustawi na mapato ya watu huko Yemen.  

COVID-19 imeongeza migogoro mingi ambayo tayari inaendelea kutokana na mzozo uliopo ambao uliozuka mwaka wa 2015, kati ya vikosi vya waasi wa Houthi, pamoja na washirika wao, na muungano unaoongozwa na Saudi, ambao unaunga mkono Serikali inayotambulika kimataifa. 

Kufikia tarehe 12 Desemba mwaka huu, kumekuwa na zaidi ya wagonjwa 10,000  wa COVID-19 walioripotiwa nchini humo, lakini ni vigumu kutathmini athari halisi kwa sababu ya upimaji mdogo na kuripoti. 

Tangu Aprili, IOM imekuwa ikiunga mkono juhudi za wizara ya afya kutoa chanjo kwa watu walio katika hatari na ambao ni vigumu kuwafikia.  

Wamejumuisha wafanyikazi wa afya, watu walio na magonjwa sugu na raia ambao ni wazee. 

Mhamiaji mmoja wa Ethiopia ambaye amepokea chanjo hiyo huko Aden, Naima Mohammed, ameliambia shirika hilo kuwa alikuwa na jamaa mmoja aliyefariki dunia kutokana na COVID-19 mwaka jana. 

Tangu wakati huo, amefika kwenye kituo cha huduma ya wahamiaji mara kadhaa ili kupata ufahamu kuhusu hatua za kujilinda, kama vile kunawa mikono na kuvaa barakoa.  "Sasa kwa kuwa nimechanjwa, nimelindwa zaidi", amesema. 

Dk Nasser Qassem Sami, mkuu wa tovuti ya ART huko Aden, Yemen, ambayo hutoa huduma za matunzo na dawa kwa watu wanaoishi na VVU
IOM/Majed M.
Dk Nasser Qassem Sami, mkuu wa tovuti ya ART huko Aden, Yemen, ambayo hutoa huduma za matunzo na dawa kwa watu wanaoishi na VVU

Mgogoro wa kiafya  

Kwa mujibu wa IOM takriban miaka saba ya mzozo nchini Yemen imedhoofisha mfumo wa afya, ambao tayari ulikuwa hatarini kabla ya virusi kufika nchini humo. 

Ugonjwa huo umekuwa na athari mbaya kwa jamii zilizotengwa zaidi ambazo hazina huduma ya afya, maji safi na vyoo. 
Kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, IOM imekuwa ikifanya vikao vya kuongeza uelewa ili kueneza taarifa sahihi na kutatua dhana potofu kuhusu chanjo. Wahamiaji waliochanjwa watapokea hati za kuwawezesha kufikia vituo vya afya kwa urahisi. 
Tangu kuanza kwa janga hili, IOM imesaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kutoa matibabu kwa walioambukizwa. 

Hadi sasa mwaka huu, zaidi ya watu 135,000 wamefikiwa na kampoeni ya uelimishaji na uhamasishaji na zaidi ya watu 400,000 wamepimwa virusi kwenye vituo vya afya vinavyosaidiwa na IOM. 

Kampeni hiyo mpya ya chanjo inatekelezwa kwa ushirikiano na wizara ya afya na shirika la afya duniani WHO kwa msaada kutoka kwa serikali za Ujerumani, Finland na mpango wa msaada wa kibinadamu wa Muungano wa Ulaya EU. 

Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.
IOM/Rami Ibrahim
Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.

Asilimia 80% wanategemea misaada 

IOM inasema vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen vimezua mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu na maendeleo duniani na kuacha sehemu za nchi hiyo zikikabiliwa na njaa. 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu, OCHA, imekadiria kuwa asilimia 80 ya watu, au watu milioni 24, wanategemea misaada na usaidizi wa ulinzi, ikiwa ni pamoja na watu milioni 14.3 ambao wanahitaji sana msaada huo. 

Kufuatia kuzuka kwa mzozo huo mwaka 2015, Umoja wa Mataifa umekuwa ukisistiza mara kwa mara kwamba hakuna suluhu ya kijeshi kwa mgogoro wa Yemen na umetoa wito wa kurejeshwa kwa mazungumzo ya amani, kupitia ofisi ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo.