Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joyce Msuya kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na kaimu wa OCHA

Naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Joyce Msuya -Kutoka Maktaba
UN Environment
Naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Joyce Msuya -Kutoka Maktaba

Joyce Msuya kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na kaimu wa OCHA

Masuala ya UM

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo metangaza kumteua Bi Joyce Msuya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa msaidizi wa wa Katibu Mkuu kwa masuala ya kibinadamu na naibu mratibu wa misaada ya dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA. 

Bi. Msuya anachukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Ursula Mueller kutoka Ujerumani ambaye Kastibu Mkuu amemshukuru kwa uongozi wake na kujitoa kwake katika muda wote wa uongozi wake. 

Guterres pia amemshukru Ramesh Rajasingham ambaye amekuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Machi 2020.  

Joyce Msuya kwenye UN 

Tangu mwaka 2018 Bi.Msuya amekuwa akihudumu kama msaidizi wa Katibu Mkuu na naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP lenye makao yake makuu mjini Nairobi Kenya . 

Akiwa katika nafasi hiyo Bi. Msuya aliwajibika na bajeti ya dola milioni 455 na mlolongo wa miradi iliyogharibu takribani zaidi yad ola bilioni 1 ambayo imetekelezwa kupitia wafanyakazi 2,500 katika ofisi 41 na makao makuu. 

Miongoni mwa kazi zingine alizofanya ni kutoa uongozi wa kiutawala kwa Sekretarieti 18 za mikataba ya mazingira ya kimataifa, ikijumuisha mikataba ya kikanda ya masuala ya bahari.  

Kati ya mwaka wa 2018 na 2019, alihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa muda katika ngazi ya msaidizi wa Katibu Mkuu, akiongoza shirika hilo kuelekea utulivu, na pia kuongoza kikao cha nne cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa na kuhamasisha rasilimali ili kusaidia kazi yake. 

Bi. Msuya anachukua wadhifa huu mpya akija na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ya katika masuala ya maendeleo ya kimataifa na fedha, mkakati unaohusisha utendakazi na ushirikiano, na uzoefu wa kufanya kazi katika sehemu mbalimbali barani Afrika, Amerika Kusini na Asia.  

Bi Msuya amewahi kushika nyadhifa kadhaa za juu za uongozi kwenye Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kuwa mwakilishi maalum na mkuu wa ofisi ya Benki ya Dunia nchini Jamhuri ya Korea, mratibu wa kanda katika taasisi ya Benki ya Dunia yenye makao yake makuu nchini China na mshauri maalum wa makamu wa Rais mwandamizi na mchumi mkuu. 

Bi. Msuya pia amewahi kuongoza mkakati na uendeshaji wa shirika la fedha la kimataifa IMF Amerika ya Kusini na Afrika, ukishughulikia sekta ya viwanda, biashara ya kilimo na huduma. 

Raia wa Tanzania, Bi. Msuya ana shahada ya uzamili ya Sayansi ya Mikrobiolojia na Kinga kutoka chuo kikuu cha Ottawa, Canada, na shahada ya kwanza ya sayansi ya Biokemia na kinga kutoka chuo kikuu cha Strathclyde, Scotland.  

Anazungumza kwa ufasaha Kiingereza, Kiswahili na Kipare.