WHO na St.Judes kusaidia zaidi ya watoto 120,000 wanaougua saratani

13 Disemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO na Hospitali ya Utafiti ya Watoto ya St. Jude hii wametangaza mipango ya kuanzisha jukwaa ambalo litaongeza kwa kasi upatikanaji wa dawa za saratani ya watoto duniani kote.

Jukwaa hilo la Kimataifa la Upatikanaji wa Dawa za Saratani ya utotoni, la kwanza la aina yake, litasaidia usambazaji usiona bughudha wa dawa za saratani ya utotoni zilizohakikiwa kuwa na ubora, kwa nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Hospitali ya St. Jude imeeleza kuwa inafanya uwekezaji wa miaka sita wa dola milioni 200.

Akizungumza katika uzinduzi wa jukwaa hili Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema karibu watoto tisa kati ya kumi walio na saratani wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati hivyo uwekezaji wa hospitali ya St.jude kwa miaka sita wa dola milioni 200 pamoja na mambo mengine utatoa dawa bila gharama kwa nchi zinazoshiriki katika awamu ya majaribio.

“Uwekezano wa kuwa na uhai baada ya kupata saratani katika nchi hizi ni chini ya 30%, ikilinganishwa na 80% katika nchi zenye kipato ya juu. Jukwaa hili jipya, ambalo linajengwa juu ya mafanikio ya Mpango wa Kimataifa wa Saratani ya Utotoni uliozinduliwa na st.Jude mwaka 2018, litasaidia kurekebisha usawa huu usiokubalika na kutoa matumaini kwa maelfu ya wazazi wanaokabiliwa na hali mbaya yakuwa na  mtoto aliye na saratani.” 

Jukwaa hilo jipya linalenga kutoa dawa salama na zinazofaa za saratani kwa takriban watoto 120,000 kati kipindi cha kuanzia mwaka 2022 mpaka 2027, huku likiwa na matarajio ya kuongezeka katika miaka ijayo.

Naye James R. Downing, MD, rais na Mkurugenzi Mtendaji wa St. Jude amesema jukwaa hili litasaidia kujenga miundombinu ili kuhakikisha watoto kila mahali wanapata dawa salama za saratani.

“St. Jude ilianzishwa kwa dhamira ya kuendeleza utafiti na matibabu ya saratani ya utotoni na magonjwa mengine mabaya ya watoto. Takriban miaka 60 baadaye, tunasimama na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, mashirika washirika na washirika wetu wa Global Alliance kupanua ahadi hiyo kwa watoto duniani kote.”

Kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na hospitali hiyo ya utafiti wa saratani za utotoni kinaelezwa kuwa ndio ahadi kubwa zaidi ya kifedha kwa sasa ulimwenguni ambayo imeahidiwa kutekeleza juhudi za kuhakikisha kuna upatikanaji wa dawa za saratani ya Watoto.

Jukwaa hili litatoa usaidizi wa mwanzo hadi mwisho wa kuunganisha mahitaji ya kimataifa ili kuunda soko, kusaidia nchi katika kuchagua dawa, kutengeneza viwango vya matibabu, na kujenga mifumo ya taarifa ili kufuatilia huduma bora inatolewa na kuendeleza uvumbuzi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter