Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwetu ni muhimu sana kuwahusisha wanawake katika ulinzi wa amani - Luteni Kanali Will Meddings

Walinda amani wa MINUSMA akiwa kwenye doria huko Gao nchini Mali
/Marco MINUSMADormino
Walinda amani wa MINUSMA akiwa kwenye doria huko Gao nchini Mali

Kwetu ni muhimu sana kuwahusisha wanawake katika ulinzi wa amani - Luteni Kanali Will Meddings

Wanawake

Kikosi cha wanajeshi kutoka Uingereza cha upelezi wa masafa marefu au LRRG chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani nchini Mali, MINUSMA kinajivunia kuwa na askari wanawake miongoni mwao kwani kutokana na uwezo wao wa kuchapa kazi nyingi na kueleweka kwa wanajamii kirahisi. John Kibego anayo maelezo zaidi. 

Ni Luteni Kanali Will Meddings akieleza kwa ufupi shughuli za kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha upelelezi wa masafa marefu chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani nchini Mali, MINUSMA. Anasema, “shughuli maalumu ya kikosi cha upelelezi wa masafa marefu ni kama jina lake linavyoweza kupendekeza kwamba ni uwezo wa kwenda umbali mrefu kukaa kwa muda mrefu na kutoa taarifa za upelelezi kwa Kamanda wa kikosi na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa lakini sio upelelezi tu pia kuchukua hatua na hivyo kama kikosi tunaenda umbali mrefu kutoka kwenye kambi yetu iliyoko Gao tunakaa huko tunakoenda kwa muda mrefu sio tu kuangalia hali ilivyo lakini pia kuwalinda raia.” 

Mnamo mwezi Agosti mwaka huu katika maeneo ya Ouatagouna kusini mashariki mwa Mali, kundi la wanaume wenye silaha walivamia vijiji na kuwaua watu kadhaa. Inafahamika kuwa makundi yenye kujihami kwa silaha na ambayo yana uhusiano na makundi ya Daesh na al-Qaeda yanaendesha shughuli zake katika maeneo hayo ndio maana kikosi hiki cha uingereza chini ya Umoja wa Mataifa kikapelekwa huko haraka wakiwa na magari yaliyoundwa maalumu kwa ajili ya mazingira ya jangwa. 

Meja Harry Wills kutoka kikosi hicho anafafanua zaidi akisema,“LRRG ni mchango wa Uingereza kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani nchini Mali. Imeundwa na vipengele tofautitofauti lakini kimsingi ni kikosi cha magari kinachoturuhusu kwenda zaidi katika maeneo ambayo hapo awali hakujawa na vikosi vya usalama vya nchi mwenyeji. Kwa hivyo kuna vipengele kadhaa hapa kwa ajili ya masafa marefu lakini pia muda ambao wanakaa huko nje. Na haya ndio mambo yetu ya kuvutia yanayoturuhusu kuwahudumia watu wa Mali kwa kuelewa matatizo yao ya kiusalama na kuufahamisha Umoja wa Mataifa ili waweze kuandaa suluhisho mahususi la kiusalama kwa ajili ya watu hawa.” 

Kikosi hiki kinajivunia kuwa na askari wanawake miongoni mwao. Wanachapa kazi na ni rahisi pia kuamini na jamii kama anavyoeleza Luteni Kanali Will Meddings,“kabisa kwetu ni muhimu sana kuwahusisha wanawake pia katika ulinzi wa amani na inafanya vitu kadhaa kwa ajili yetu. Kwanza inamaanisha kuwa tunaweza kuzungumza na wanaume na wanawake kwa usawa tunapokuwa kwenye doria. Hatuna timu maalumu za wanawake katika kikosi chetu bali tuliona ni wanawake katika kikosi chetu kwa ujumla na hiyo inamaanisha kila tunakoenda tunaweza kuzungumza na wanaume na wanawake, tunaweza kuongea na watoto na tulichogundua ni kwamba kuwa na askari wa ardhini ambao ni wanawake ni nzuri sana kwetu kuondoa vizuizi kwa kuelewa matatizo ambayo huwezi kuingia kwenye nchi kama hii ambayo kumekuwa na matatizo ya mapigano na vurugu na kwa hivyo wanaume wakati mwingine wanaweza kuonekana kuwa wa kutisha. ” 

Private Samuel ni mmoja wa wanajeshi wanawake katika kikosi hiki anaeleza changamoto ambayo wasichana wengi wanakumbana nayo duniani kote,“ilikuwa ndoto yangu ya utoto ambayo nilikuwa nayo kwamba wakati wote nilitaka kujiunga na jeshi la ardhini. Marafiki zangu nyumbani walisema huwezi kujiunga na jeshi kwa kuwa hiyo ni kazi ya wanaume watupu. Nikawaambia niangalieni mimi, jeshi linaruhusu wanawake nitajiunga na nitakamilisha mafunzo. Sasa niko hapa nimefanya na niko hapa Mali kwenye operesheni.” 

Koplo Gwilliam ni mwanamke mwingine katika kikosi hiki anasema,“ninajiona kama askari tu na niko hapa kufanya kazi iwe ya kiume iwe ya kike hicho ndicho ninachokiona. Kama mwanaume au mwanamke sio kila siku iko sawa. Ni tofauti kila siku. Kwa hivyo utakuta kazi fulani kwa mfano ya kurekebisha gari, ina dalili zile zile lakini tatizo tofauti.” 

Kama anavyosema Koplo Gwillian, wanawake katika kikosi hiki wanachapa kazi za kila namna. Katika video iliyoandaliwa na MINUSMA, mwanajeshi huyu anaonekana akifunga tairi la gari kubwa la kijeshi. Na katika mazingira mengine wote wanashirikiana katika kuandaa na kurusha ndege zisizo na rubani ili ziende mbali kwenda kuleta picha, video na taarifa kadha za kiusalama.  Luteni Kanali Will Meddings anatoa maelezo kuhusu hili, “hii ni moja ya uwezo ambao ninafikiri tunaweza kusema ni sehemu ya yanayohitajika kwa vikosi vya kisasa vya ulinzi wa amani. Wazo la mpango wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ilikuwa kusimama kwenye ukuta katikati ya makundi mawili yenye silaha nadhani imepitwa na wakati na ulinzi wa amani wa kisasa unahitaji vitu kama ndege zisizo na rubani, unahitaji upelelezi. Hizi sio teknolojia za juu sana lakini kwetu zinaturuhusu kuona mbali kuliko macho yetu yanakoweza kuona kama kilomita 20 hadi 30 muhimu kuwalinda raia katika eneo kubwa.” 

Kwa upande wake Meja Harry Wills akihitimisha makala yetu hii ya leo anaeleza wote wanavyojivunia kushiriki katika ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa,“MINUSMA ina mchanganyiko kutoka kote duniani. Na kuna nchi nyingi zinazochangia vikosi. Ninafikiri hisia kubwa ni kujivunia kuwa sehemu ya huduma hiyo. Kwa hivyo tuko hapa, kuwalinda raia na tuko hapa kwa ulinzi wa amani.”