Ili kudumisha haki ni muhimu kujenga imani, kudumisha uhuru na kuhakikisha usawa :UN

10 Disemba 2021

Leo ni siku ya Haki za binadamu, ambapo wito umetolewa kwa kila mmoja kuunga mkono juhudi za kuimarisha usawa kwa kila mtu kila mahali, ili tuweze kupata nafuu bora, ya haki na matumaini mapya pamoja na kujenga upya jamii ambazo ni thabiti na endelevu zaidi katika kujali haki.

Katika taarifa yake kuhusu siku hii kamishina mkuu wa haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema licha ya mafanikio makubwa tangu kupitishwa kwa Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu miaka 73 iliyopita, janga la COVID limeonesha ongezeko la kutisha la ukosefu wa usawa. 

Bi. Bachelet na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wameitumia fursa ya siku ya leo kutathmini maendeleo yaliyopatikana, yale dunia iliyojifunza  , na kuweka mbele ajenda mpya ya amani inayowasilisha maono na usalama wa kimataifa. 

"Hii ni ajenda ya utekelezaji na ajenda ya haki," amesema Bi. Bachelet na kuongeza kuwa “Ajenda yetu ya pamoja” mfumo uliowekwa na Katibu Mkuu mwezi Septemba mwaka huu 2021 ni mkataba mpya wa kijamii unaozingatia haki za binadamu na unaotaka mshikamano mpya kote duniani. 

Agenda hiyo inapendekeza kuimarisha hatua za pamoja kwa  ajili ya kushughulikia sababu kuu za ukosefu wa usalama, kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kujenga mnepo na ya tahadhari ya mapema, kuendeleza ushirikiano wa kimataifa, na juhudi endelevu zaidi katika ujenzi wa amani na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Hatua zilizopigwa zi mashakani 

Bi Bachelet ameweka bayana kwamba kwamba tangu azimio la kimataifa la haki za binadamu (UDHR) lilipotiwa saini kwa mara ya kwanza, “Dunia kwa ujumla imezidi kuwa tajiri, na watu wanaishi muda mrefu zaidi. Watoto zaidi wanaenda shule, na wanawake zaidi wameweza kupata kwa kiasi kubwa uhuru. Watu wengi zaidi katika nchi nyingi wamekuwa na fursa zaidi za kuvunja minyororo ya umaskini, matabaka, ubaguzi na jinsia.” 

Hata hivyo amesisitioza kwamba licha ya maendeleo yote haya majanga na misukosuko iliyoikumba dunia katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, mfululizo na kuzuka kwa janga hili la COVIDF-19 mwaka 2020 kumedhoofisha maendeleo haya.

Akina mama wa Mexico ambao binti zao wamekuwa waathiriwa wa mauaji ya wanawake wanadai haki.
Primavera Diaz
Akina mama wa Mexico ambao binti zao wamekuwa waathiriwa wa mauaji ya wanawake wanadai haki.

Tishio jipya kwa haki za binadamu:Guterres 

Huku dunia ikiwa katika njia panda, vitisho vipya vimeibuka dhidi ya haki za msingi za binadamu, kama vile janga la COVID-19, teknolojia ya kidijitali, na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, amesema leo Katibu Mkuu Guterres, katika ujumbe wake kwa siku hii ya haki za binadamu inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 10. 

Ameongeza kuwa "Nafasi ya umma inapungua. Umaskini na njaa vinaongezeka kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa. Mamilioni ya watoto wanakosa haki yao ya kupata elimu. Ukosefu wa usawa unaongezeka lakini tunaweza kuchagua njia tofauti”. 

Bwana Guterres amebainisha kuwa kujikwamua kutokana na janga la COVID-19 "lazima iwe ni fursa ya kupanua wigo wa haki za binadamu na uhuru, na kujenga upya uaminifu. Imani inahitaji kurejeshwa katika mifumo ya haki na kutopendelea kwa kutumia sheria na taasisi kila mahali, pia utu unapaswa kurejeshwa, pamoja na imani kwamba watu wanaweza kusikilizwa kwa haki, na kutatua malalamiko yao kwa amani.” 

Bwana Guterres akaenda mbali zaidi na kuongeza kuwa "Umoja wa Mataifa unasimamia haki za kila mwanachama wa familia yetu ya kibinadamu. Leo na kila siku, tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya haki, usawa, utu na haki za binadamu kwa wote." 

Waandamanaji katika maandamano ya Amani na Uhuru huko Minsk, Belarus (picha ya faili).
Unsplash/Andrew Keymaster
Waandamanaji katika maandamano ya Amani na Uhuru huko Minsk, Belarus (picha ya faili).

 

Usawa, na faida kwa wote 

Bi. Bachelet, amemalizia taarifa yake akisema usawa ulikuwa "kiini cha haki za binadamu. Usawa ni juu ya huruma na mshikamano na juu ya kuelewa kwamba, kama binadamu wa kawaida, njia yetu pekee ya kusonga mbele ni kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote." 

Kwa mantiki hiyo ameongeza kuwa imeeleweka vyema katika kipindi cha ujenzi mpya wa dunia baada ya vita kuu ya pili ya dunia. 

"Hata hivyo, kushindwa kwetu kujiimarisha vyema baada ya mgogoro wa kifedha muongo mmoja uliopita, pamoja na msukosuko wa kijamii na kiuchumi unaosababishwa na janga la COVID-19 na athari zinazoongezeka kwa kasi za mabadiliko ya tabianchi, kunaonyesha kuwa tumesahau suluhu zilizo wazi na zilizothibitishwa zinazotokana na binadamu. haki na umuhimu wa kukabiliana na ukosefu wa usawa.” 

Ikiwa maendeleo yatadumishwa, somo hilo la msingi twahitaji kujifunza kwa mara nyingine tena, “si kwa ajili ya wale tu wanaoteseka kutokana na ukosefu mkubwa wa usawa unaoikumba dunia yetu, bali kwa ajili yetu sote”. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter