WHO yashauri nchi za kipato cha chini na cha kati kuwekeza katika magonjwa yasiyoambukiza

13 Disemba 2021

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO inaonesha karibu vifo milioni saba vinaweza kuzuiwa ifikapo mwaka 2030, ikiwa nchi za kipato cha chini na cha kati zingewekeza chini ya dola moja kwa kila mwananchi kwa mwaka katika kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukiza.

Ripoti hiyo imepewa jina “Kuokoa maisha, kutumia kidogo: mfano wa kuwekeza katika magonjwa yasiyoambukiza unaweka kuwa ni njia ambayo nchi zinaweza kufuata ili kizazi kiwe bora na chenye afya. 

Akisoma ripoti hiyo mbele ya vyombo vya habari mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kwa uwekezaji sahihi wa kimkakati, nchi ambazo zinabeba kiasi kikubwa cha mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza zinaweza kubadilisha mwelekeo wao wa magonjwa na kuleta faida kubwa za kiafya na kiuchumi kwa raia wao.

“Katika ulimwengu uliojaa kutokuwa na uhakika, jambo moja tunaloweza kuwa na uhakika nalo ni kwamba bila kuchukua hatua, magonjwa yasiyo ya kuambukiza yataendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya kimataifa. Kuwekeza katika sera hizi zenye msingi wa ushahidi ni uwekezaji mzuri wa afya kwa siku zijazo.”

Magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na ugonjwa wa moyo, kisukari, saratani, na magonjwa ya kupumua, ambayo yamekuwa yakisababisha vifo saba kati ya vifo kumi kote ulimwenguni.

Hata hivyo athari zao kwa nchi za kipato cha chini mara nyingi hazizingatiwi, licha ya ukweli kwamba asilimia 85 ya vifo vya mapema (kati ya umri wa miaka 30-69) kutokana na magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na kuzifanya kuwa na mzigo mkubwa wa afya, kijamii na kiuchumi.

Muuguzi akimuonesha mkimbizi wa Kipalestina nchini Jordan programu ya afya kwenye simu yake ya mkononi
© UNRWA/George Awwad
Muuguzi akimuonesha mkimbizi wa Kipalestina nchini Jordan programu ya afya kwenye simu yake ya mkononi

Suluhisho la magonjwa yasiyoambukiza

Idadi kubwa ya vifo hivyo vinaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zilizopendekezwa na WHO zilizojaribiwa na kuonekana zitafaa kutumika.

WHO imezitaja njia hizo kuwa ni pamoja na hatua za gharama nafuu za kupunguza matumizi ya tumbaku na matumizi mabaya ya pombe, kuboresha lishe, kuongeza mazoezi ya mwili, kupunguza hatari za magonjwa ya moyo na mishipa, kisukari, na kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.

Ripoti hiyo inasisitiza udharura wa kuwekeza katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikizingatiwa kwamba janga la COVID-19 limeonesha  namna magonjwa hayo yanavyoweza kuzidisha hatari.

Naye balozi wa Kimataifa wa WHO kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na Majeruhi Michael R. Bloomberg amesema  “Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaathiri vibaya afya na uchumi, hasa kwa nchi ambazo hazina uwezo wa kumudu. Tunajua hatua za kuzuia zinazofanya kazi vizuri zaidi, na tunatumai ripoti hii mpya itaziongoza serikali zaidi kuchukua hatua nzuri na za gharama nafuu ambazo zinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote.”

Kwa kuwekeza katika sera 16 zinazopendekezwa na WHO, nchi hazitalinda tu watu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, lakini pia zitapunguza athari za magonjwa ya kuambukiza kama COVID-19 katika siku zijazo.

Njia hizo zinazopendekezwa tayari zimetumika kwa mafanikio katika nchi nyingi duniani, hauku kukiwa na mafanikio makubwa yaliyoambatanishwa kwenye ripoti hiyo.

Wafadhili wa kimataifa pia wameanza kutumia hoja hizo ili kuchochea uwekezaji katika eneo hilo, mwaka 2019 Serikali ya Norway ilizindua mkakati wa kwanza wa maendeleo wa kimataifa kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter