Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rushwa katika michezo, kamari zawavutia zaidi wahalifu na kutumia michezo vibaya

Uwanja wa michezo New York
UN News/ Anton Uspensky
Uwanja wa michezo New York

Rushwa katika michezo, kamari zawavutia zaidi wahalifu na kutumia michezo vibaya

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Zaidi ya dola trilioni 1.7 zinakadiriwa kuuzwa kwenye soko haramu za kamari kila mwaka, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti madawa na uhalifu, UNODC.

Ripoti hiyo inazinduliwa leo huko Vienna Austria ikiwa ni siku chache tuu kabla ya kuanza kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na rushwa utakaofanyika Sharm El-Sheikh, Misri kuanzia tarehe 13 hadi 17 Disemba, ambapo suala la rushwa kwenye michezo litajadiliwa.

Ingawa rushwa katika michezo si jambo geni,  shughuli za ulaghai katika uendeshaji wa taasisi za michezo na mashindano zimekuwa zikirekodiwa tangu enzi za michezo ya Olimpiki ya kale, lakini katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kimeshuhudia ongezeko kubwa la uhalifu katika eneo hili. 

Ikiwa imetengenezwa kwa ushirikiano na takriban wataalam 200 kutoka serikalini, mashirika ya michezo, sekta ya kibinafsi, wasomi, na wadau wengine mbalimbali  imekuwa ripoti yenye kueleza kwa kina zaidi masuala ya rushwa na namna yanavyotokea. 

Hakika, utandawazi, utitiri mkubwa wa fedha kwenye ukuaji wa kasi wa kamari halali na haramu kwenye michezo, na maendeleo ya kiteknolojia kumebadilisha jinsi mchezo unavyochezwa na kutumika na kuufanya uvutie zaidi kwa mitandao ya wahalifu inayotafuta kutumia michezo kwa faida isiyo halali.

Yaliyomo kwenye ripoti

Ripoti hiyo inatoka katika wakati muhimu, kukiwa na kuongezeka kwa msisitizo wa juhudi za kupambana na rushwa katika sekta zote, ikiwa ni pamoja na sekta ya michezo.

Pamoja na kueleza kinaga ubaga namna uhalifu unavyofanyika katika sekta ya michezo, ripoti hiyo imeandika kama kitabu kinachoeleza namna madhubuti ya kukabiliana na uhalifu na ufisadi kwa kuweka sera madubuti, ripoti hiyo ya Kimataifa ya Ufisadi katika Michezo pia inafichua kiwango cha kushangaza, udhihirisho, na utata wa rushwa na uhalifu uliopangwa katika michezo duniani, kikanda, na katika ngazi za kitaifa.

Ripoti hiyo ya rushwa katika michezo imechanganua dhima mbalimbali zikiwemo;- kamari haramu,udanganyifu katika shindano, unyanyasaji katika michezo, uwezekano wa kung’amua matukio makubwa ya ufisadi katika michezo, na ushiriki wa uhalifu uliopangwa, miongoni mwa mengine.

Pia imeangazia mabadiliko ya mazingira ya michezo na uhusiano wake na vitendo vya rushwa, mipango iliyopo ya kukabiliana na tatizo hilo, masuala yanayohusiana na kugundua na kuripoti makosa, pamoja na jinsi mifumo iliyopo ya kisheria inaweza kutumika kushughulikia rushwa katika maeneo hayo.

Masuala ya kufanyia kazi kwa dharura

Miongozo hii imetengenezwa ikilenga serikali na mashirika ya michezo 

•    Kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuzuia na kukabiliana na mbinu tofauti za rushwa na uhalifu katika michezo katika ngazi ya kimataifa, kikanda na kitaifa.
•    Kutengeneza na kutekeleza sera za kupinga ufisadi katika michezo, kwa kuzingatia kushughulikia ufisadi unaohusishwa na uandaaji wa hafla kuu za michezo, mashindano yenye udanganyifu, kamari haramu, na ushiriki wa uhalifu uliopangwa katika michezo.
•    Kukuza na kuongeza ushirikiano na ubadilishanaji wa taarifa na mazoea mazuri kati ya mashirika ya michezo, mamlaka za kuzuia uhalifu na makosa ya jinai, watunga sheria na watunga sera.
•    Kukuza uelewa wa vitu vinavyunganisha rushwa na uhalifu wakupangwa katika michezo na kutengeneza taasisi husika za serikali na mashirika ya michezo zakuwashughulikia.