Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzoefu tuliopata katika kukagua UN umetuwezesha kuimarisha ukaguzi wa mifumo Tanzania: Kichere

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Tanzania Charles Edward Kichere (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa UN News Kiswahili (kushoto)
Assumpta Massoi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Tanzania Charles Edward Kichere (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa UN News Kiswahili (kushoto)

Uzoefu tuliopata katika kukagua UN umetuwezesha kuimarisha ukaguzi wa mifumo Tanzania: Kichere

Masuala ya UM

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanzania Charles Kichere amesema miaka 9 ya Tanzania kushiriki kwenye bodi ya ukaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa umekuwa na manufaa makubwa kwa watendaji wake kwani wamepata ujuzi mkubwa wa mifumo ya fedha. 

Akizungumza na Leah Mushi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa Kichere amesema uzoefu huo tayari umeanza kuzaa matunda kwani wamekuwa wakipata kazi mbalimbali barani Afrika ambazo zimewataka kujikita katika kukagua misheni za kivita, uzoefu waliopata Umoja wa Mataifa. 

“Katika kipindi chetu chakuwa wakaguzi kwa miaka 6 na kuwa waangalizi katika jopo la wakaguzi kwa miaka 3 jumla miaka 9 tumenufaika sana, kwanza ilianza kama changamoto maana watendaji wangu walikuwa wanaenda kukagua misheni za umoja wa mataifa, haya ni maeneo ya vita kama Afghanistan, Lebanon, Somalia na Darfur huku tukilindwa na askari wa umoja wa Mataifa lakini sasa nchi nyingi Afrika zinatutambua kama wabobezi katika ukaguzi wamaeneo hayo.” 

Kichere ambaye tarehe 08 Desemba 2021 katika mkutano wa 61 wa jopo la wakaguzi wa Umoja wa Mataifa na taasisi zake alitoa hotuba yake rasmi ya kuaga kuwa mjumbe wa bodi tangu Tanzania ilivyoingia katika bodi hiyo rasmi mwaka 2012 amesema wanaondoka na ujuzi mkubwa sana.

“Kuwepo katika chombo hiki cha Umoja wa Mataifa kumetusaidia kama nchi kuelewa nini kinafanyika na kuongeza ujuzi wetu katika mambo ya ukaguzi na huku kama Tanzania tukichangia kutoa ushauri mbalimbali, tumetoa mchango mkubwa lakini na sisi tumepata ujuzi mkubwa sana na ujuzi huu tunaupeleka nyumbani sasa.”

Nini wanapeleka Tanzania

Mdhibiti na Mkaguzi huyu Mkuu wa Serikali ya Tanzania akieleza nini hasa wanaondoka nacho amesema 
“Hawa wenzetu wapo mbele zaidi kwenye masuala ya mifumo , ukaguzi wa kukagua mifumo, kukagua mashirika na mifumo yao kwakweli iko juu sana. Kwahiyo na sisi tumejifunza sana kukagua mambo ya mifumo hasa kwahiyo tumejenga utaalamu mkubwa sana kwenye kukagua mifumo.” 

Kichere amesema uzoefu huo umewajengea uwezo mkubwa sana vijana wa ofisi yake na nyumbani sasa wataenda kukagua vizuri zaidi, ukaguzi utazidi kuimarika kutokana na kujifunza kutoka maeneo mbalimbali wakati wa jukumu lao ndani ya Umoja wa Mataifa. 

Changamoto

Suala la ukaguzi wa Umoja wa Mataifa pamoja na kuwa ni fursa kubwa lakini Ukaguzi ndani ya nchi yao ni suala la kikatiba hivyo walilazimika kufanya kazi sehemu zote kwa ufanisi mkubwa. 

“Tuna matakwa yetu ya kikatiba kwanza lazima tukague mahakama, serikali, Bunge na mashirikia ya umma na kila kitu kwahiyo unakuta idadi yetu ni kidogo kwahiyo lazima kuwe na ulinganifu, ukague Umoja wa Mataifa na kukagua nyumbani na kutoa ripoti kwahiyo tulijitahidi kufanya vyote na tukafanikiwa na kutoa taarifa kwa umakini na kwa wakati.”

Vijana ndani ya Ofisi ya CAG

Kichere amewapongeza vijana wa ofisi yake kwasababu “wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba tunatimiza majukumu ya nyumbani na majukumu ya Umoja wa Mataifa bila kuangushana sehemu yoyote.”

Kazi hii pia umejenga uwezo kwa vijana wetu “Ilibidi tujenge uwezo mkubwa sana kwa vijana wetu, nilikuwa nawaambia kwamba huu ukaguzi wa Umoja wa Mataifa unagharamiwa na Umoja wa Mataifa wenyewe kwahiyo tumetumia rasilimali ambazo tulikuwa tunapata kuwajengea uwezo vijana wetu. Vijana wetu wapo vizuri tulikuwa na changamoto za uwezo mwanzoni lakini tumeujenga umekuwa mzuri.”

Wakati wa ukaguzi vijana walikuwa wanaenda kwenye misheni za Umoja wa Mataifa wanakagua huku wamesimamiwa na mitutu wakilindwa na askari wa Umoja wa Mataifa wameenda maeneo kama Somalia na Lebabon na wanakutana na chagamoto mbalimbali lakini Umoja wa Mataifa ukawa unasaidia maeneo yote hayo na vijana wakawa wanalindwa vizuri. 

Mipango ya baadae

CAG Charles kichere amesema baada ya kumaliza kuhudumu wanatakiwa kuondoka lakini wanao uwezo wa kurudi tena kuomba kukagua Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Amesema ili jambo hilo liweze kutimia kunahitajika ushirikiano mkubwa wa taasisi mbalimbali za Tanzania. 

‘Katika bodi kuna mifano ya nchi ambazo zilitoka na kurudi kama vile China, na sisi tunaweza kurudi, sisi tutaomba hizo kazi tena baadae, anayechaguliwa kwenye ukaguzi sio CAG bali ni nchi kwahiyo hii inataka na chi yenyewe ijiweke tayari kuwa nafasi zikitoka na yenyewe itusaidie kwakuwa hii ni nafasi kubwa sana. Serikali inasaidia kwa maana ya wenzetu Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, lakini na nyumbani pia. Na nimeshawasiliana nao kuona jinsia ambavyo tunaweza tukafanya maana tumeshapata uzoefu.”

Kichere pia anasema katika hotuba yake ya kuwaaga wajumbe wa bodi ya ukaguzi aliwaomba wajumbe waliobaki kuwa iwapo nafasi ikitokea na Tanzania wakaomba ameomba wasisite kuwasaidia ili waweze kurudi. 

Mchango wa CAG watangulizi 

Pia amewashukuru watangulizi wenzake wa nafasi ya CAG kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwezesha kufikia walipo sasa. “Mzee Ludovic Utou akiwa CAG yeye ndio aliwezesha Tanzania kuingia Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza mwaka 2012. Alivyotoka akamuachia Profesa Mussa Assad ambaye alifanya kazi nzuri, alikuwa ni mwenyekiti wa jopo mwaka 2016 na 2017 baada ya yeye kutoka ndio mimi nikaingia. 

Ameongeza kuwa “Hawa wenzangu kusema kweli walijenga misingi mizuri ya kuwezesha kuingia katika jopo na sasa tunapata nafasi ya kuitangaza Tanzania katika eneo la Ukaguzi wa hesabu na tunapata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali baada ya kupata hii fursa ya kukagua Umoja wa Mataifa.”