Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na wadau Tanzania wapongeza uamuzi wa serikali kurejesha shuleni watoto waliopata ujauzito

Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia
UN Women Tanzania/Deepika Nath
Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia

UNICEF na wadau Tanzania wapongeza uamuzi wa serikali kurejesha shuleni watoto waliopata ujauzito

Utamaduni na Elimu

Nchini Tanzania wadau wa masuala ya haki za mtoto likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wamepongeza hatua ya serikali ya kuamua kurejesha shuleni watoto waliokatiza masomo ya elimu ya msingi na sekondari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.
 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifafanua uamuzi huo wa serikali wakati akiwa ziarani mkoani Geita ambako alisema “tumeamua, watoto wote ambao wameacha shule kwa sababu mbalimbali utoro, sababu za kisheria kwamba ukipata mimba huwezi kuruhusiwa kuendelea na masomo, na wale waliodondoka darasa la saba tunajua kuna wanafunzi wetu wazuru sana, kwa bahati mbayá wakati wa mtihani, mtihani ni mtihani, hawakufanya vizuri, lakini baada ya kukaa nje wamejutia tunawapa nafasi nyingine kurudi na na kufanya mtihani. Lengo la uamuzi huu ni  kutoa fursa pana kwa mtoto wa kitanzania kuweza kuendelea na elimu.”

Tamko hilo hasa kuhusu kurejeshwa katika mfumo rasmi wa shule watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa shuleni lilikuwa linasubiriwa kwa hamu na wadau wengi wa haki za mtoto iwe ndani na nje ya Tanzania kwa kuzingatia haki kuu nne za msingi za mtoto za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.

Uamuzi huo uko katika waraka namba 2 wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini humo uliotangazwa tarehe 24 mwezi Novemba mwaka 2021.

Miongoni mwa walionielezea hisia zao baada ya kupitishwa tamko hilo la Rais ni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Tanzania ambapo Afisa wake wa Elimu, Jinsia na Afya ya Uzazi Penina Sangiwa akafunguka kuwa ni jambo wamelipokea kwa furaha kubwa na wanapongeza serikali ya Tanzania kwa “kufanya uamuzi huo mkubwa ambao unawezesha mtoto wa Tanzania kupata haki yake ya msingi ya elimu na kuweza kukamilisha mzunguko wake wa elimu.Sote tunafahamu elimu ina faida kubwa kwa mtoto wa kike na wa kiume na kwa kupata elimu unamjengea uwezo wa kuchangia maeneo mbalimbali ya kiuchumi na pia kumuendeleza sambamba na kuingia katika kujenga taifa na kujiendeleza kama jamii au familia.”

Na akaenda mbali kuzungumzia kile kinapaswa kufanyika hivi sasa akisema ni kuweka mazingira ambamo kwayo watoto watakaorejea shuleni hawatanyanyapaliwa siyo tu shuleni bali pia kwenye jamii.

Wadau wengine ni vyombo vya habari ambapo Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri ambalo limekuwa likishirikiana na UNICEF kupaza sauti kuhusu haki za mtoto, hakuficha hisia zake.

Amesema “tunapongeza serikali kwa hatua hii lakini hatumaanishi kwamba tu watoto wakafungulie kila kitu ili waanze kupata mimba.  Ingawa tunatetea haki ya mtoto kupata elimu baada ya kupata mimba, si haki mtoto kupata mimba kabla ya utu uzima. Kwa hiyo tunasema ni fursa nzuri tunashukuru serikali kwa kusikia hiki kilio lakini hata wanafunzi nao wajitunze.”

Wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na ujauzito au utoro watarejea shuleni ndani ya miaka miwili tangu walipoacha masomo na kwamba tamko haliwahusu wale waliofukuzwa shule kutokana na makosa ya mwelekeo wa jinai au kuhatarisha amani ya shule.

Na sasa ni hatua gani basi zinapaswa kuchukuliwa ili kuepusha mimba katika umri mdogo? Harriet  Mkaanga, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la My Health Foundation nchini Tanzania amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora shuleni na nyumbani ili mtoto wa kike asipate vishawishi vya kumchochea kushiriki kwenye ngono za umri mdogo. Mathalani watoto wawe kwenye mabweni na pia wapatiwe masodo au taulo za kike kwa kuwa “wakati mwingine mtoto wa kike anajikuta kwenye uhusiano ili aweze kupata fedha za kununulia masodo.”

Na kwa UNICEF Tanzania hilo tayari wamejipanga ambapo Bi. Sangiwa amesema “tutashirikiana na serikali na wadau wengine kutoa elimu ya maisha kwa wanafunzi.”