Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumwa wa kisasa ni nini?  

Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)
UN Photo/Mark Garten)
Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)

Utumwa wa kisasa ni nini?  

Haki za binadamu

Ulimwengu hii leo ukiazimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa, takwimu za Shirika la Kazi Duniani, ILO zinasema zaidi ya watu milioni 40 duniani kote ni wahanga wa utumwa wa kisasa.  

Ingawa utumwa wa kisasa haujafafanuliwa katika sheria, unatumika kama neno mwavuli linalojumuisha vitendo kama vile kazi ya kulazimishwa, utumwa wa madeni, ndoa ya kulazimishwa na biashara haramu ya binadamu. “Kimsingi, inarejelea hali za unyonyaji ambazo mtu hawezi kukataa au kuondoka kwa sababu ya vitisho, vurugu, kulazimishwa, udanganyifu, na/au matumizi mabaya ya mamlaka.” Inasema ILO

Kama alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kuhusu maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe pili ya mwezi Desemba, “wakati wengine wanaweza kuamini utumwa kuwa kitu cha zamani, uovu huu unaendelea kuharibu ulimwengu wetu wa kisasa.” 

Takwimu za ILO zinaeleza kuwa zaidi ya watoto milioni 150 wanakabiliwa na ajira ya watoto, ikiwa ni pamoja na takribani mtoto mmoja kati ya kumi duniani kote. 

Takriban watu milioni 40.3 wako katika utumwa wa kisasa, ikiwa ni pamoja na watu milioni 24.9 katika kazi ya kulazimishwa na milioni 15.4 katika ndoa za kulazimishwa. 

“Kuna waathiriwa 5.4 wa utumwa wa kisasa kwa kila watu 1,000 ulimwenguni.” Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaeleza.  

Kati ya watu milioni 24.9 walionaswa katika kazi za kulazimishwa, watu milioni 16 wananyonywa katika sekta binafsi kama vile kazi za nyumbani, ujenzi au kilimo; Watu milioni 4.8 katika unyonyaji wa kingono wa kulazimishwa, na watu milioni 4 katika kazi ya kulazimishwa iliyowekwa na mamlaka ya serikali. 

Wanawake na wasichana wanaathiriwa zaidi na kazi ya kulazimishwa, wakichukua asilimia 99 ya waathiriwa katika tasnia ya biashara ya ngono, na asilimia 58 katika sekta zingine. 

ILO imepitisha Itifaki ya kisheria iliyoundwa ili kuimarisha juhudi za kimataifa za kuondoa kazi ya kulazimishwa, ambayo ilianza kutumika mnamo Novemba 2016. 

Aina Kuu za Utumwa wa Kisasa 

Utumwa umebadilika na kujidhihirisha kwa njia tofauti katika historia. Leo baadhi ya aina za utumwa wa kimapokeo bado zinaendelea kuwa katika namna zao za awali, huku nyingine zimegeuzwa kuwa mpya. Mashirika ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa yameandika kuendelea kwa aina za zamani za utumwa ambazo zimejikita katika imani na desturi za jadi. Aina hizi za utumwa ni matokeo ya ubaguzi wa muda mrefu dhidi ya makundi yaliyo hatarini zaidi katika jamii, kama vile zile zinazochukuliwa kuwa za tabaka la chini, makabila madogo na watu wa asili. 

Kazi za kulazimishwa 

Pamoja na aina za jadi za kazi za kulazimishwa, kama vile kazi ya dhamana ambayo mtu anawekwa kama dhaman na utumwa wa madeni, sasa kuna aina nyingi zaidi za kisasa za kazi ya kulazimishwa, kama vile wafanyakazi wahamiaji, ambao wamesafirishwa kwa unyonyaji wa kila aina ya kiuchumi katika uchumi wa dunia: kazi katika utumwa wa nyumbani, sekta ya ujenzi, sekta ya chakula na nguo, sekta ya kilimo na ukahaba wa kulazimishwa. 

Ajira kwa watoto 

Ulimwenguni, mtoto mmoja kati ya kumi anafanya kazi. Ajira nyingi za watoto zinazofanyika leo ni za unyonyaji wa kiuchumi. Hiyo ni kinyume na Mkataba wa Haki za Mtoto, unaotambua “haki ya mtoto kulindwa dhidi ya unyonyaji wa kiuchumi na kufanya kazi yoyote ambayo inaweza kuwa hatari au kuingilia elimu ya mtoto, au kuwa na madhara kwa mtoto, afya ya mtoto au ukuaji wake wa kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili au kijamii.” 

Usafirishaji haramu wa binadamu 

Kwa mujibu wa Itifaki ya Kuzuia, Kukandamiza na Kuadhibu Usafirishaji Haramu wa Binadamu hasa Wanawake na Watoto, biashara haramu ya binadamu ina maana ya kuwaajiri, kuwasafirisha, kuwahamisha, kuwahifadhi au kuwapokea watu kwa njia ya vitisho au matumizi ya nguvu au aina nyinginezo za shuruti kwa madhumuni ya unyonyaji. Unyonyaji unajumuisha ukahaba wa watu wengine au aina nyingine za unyonyaji wa kingono, kazi ya kulazimishwa au huduma, utumwa au mazoea sawa na utumwa, utumwa au kuondolewa kwa viungo. Idhini ya mtu aliyesafirishwa kwa ajili ya unyonyaji haina umuhimu na iwapo aliyesafirishwa ni mtoto, ni uhalifu hata bila kutumia nguvu. 

Siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomezwa utumwa huadhimishwa kila mwaka tarehe 2 Desemba, tarehe ambayo ulianza kutekelezwa mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu na unyonyaji kupitia ukahawa kwa watu wengine. Mkataba huo ulianza kutekeleza rasmi mwaka 1951.