Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika yaongeza nguvu kudhibiti Omicron 

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO limeonya kuwa Omicron inaweka hatari kubwa zaidi ya maambukizo kuongezeka kote ulimwenguni.
WHO
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO limeonya kuwa Omicron inaweka hatari kubwa zaidi ya maambukizo kuongezeka kote ulimwenguni.

Afrika yaongeza nguvu kudhibiti Omicron 

Afya

Taarifa ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO Kanda ya Afrika iliyotolewa hii leo Desemba 2 mjini Brazzaville, Congo, inasema nchi za Kiafrika zinaongeza hatua za kugundua na kudhibiti kuenea kwa mnyumbuliko mpya wa virusi vya corona, Omicron huku maambukizi mapya ya Covid -19 yakiongezeka kila wiki katika bara hilo kwa asilimia 54 kutokana na kuongezeka nchini Afrika Kusini. 

Kwa mujibu wa WHO Afrika, mnyumbuliko mpya wa virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, Omicron sasa umegunduliwa katika nchi nne, huku Ghana na Nigeria zikiwa nchi za kwanza za Afrika Magharibi na za hivi karibuni zaidi barani humo kuripoti aina hiyo mpya ya virusi. Hadi kufikia sasa, Botswana na Afrika Kusini zimeripoti maambukizi ya Omicron, Botswana ikiwa na wagonjwa 19 na Afrika Kusini ikiwa na wagonjwa 172. Takwimu za dunia zinaonesha kuwa zaidi ya nchi 20 zimeshagundua uwepo wa Omicron uku nchi hizo mbili za kusini mwa Afrika, zikichangia kwa asilimia 62 za maambukizi yote ya Omicron yaliyoripotiwa ulimweni.  

Watafiti na wanasayansi nchini Afrika Kusini na eneo hilo wanazidisha uchunguzi wao ili kuelewa uambukizaji, ukali na athari za Omicron kuhusiana na chanjo zinazopatikana, uchunguzi na matibabu na kama inachochea ongezeko la hivi karibuni la maambukizi ya COVID-19

Kwa kufanya kazi na serikali za Afrika ili kuharakisha utafiti na kuimarisha mwitikio wa mnyumbuliko mpya, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO linahimiza nchi kufanya kati ya sampuli 75 na 150 kila wiki. 

Dkt Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amenukuliwa akisema, "kugunduliwa na kuripoti kwa wakati kwa mnyumbuliko mpya wa virusi Botswana na Afrika Kusini kumenunua wakati wa ulimwengu. Tunayo fursa lakini lazima tuchukue hatua haraka na kuongeza hatua za ugunduzi na uzuiaji. Nchi lazima zirekebishe mwitikio wao wa COVID-19 na kukomesha kuongezeka kwa maambukizi kuenea kote barani Afrika na pengine kuzidisha mzigo kwa  vituo vya afya ambavyo tayari vimeelemewa. "  

Nchini Afrika Kusini, WHO inatuma timu katika Jimbo la Gauteng kusaidia ufuatiliaji wa watu walioambukizwa na pia wale waliokutana nao, kuzuia maambukizi na hatua za matibabu. Botswana inakuza uzalishaji na usambazaji wa oksijeni, ambayo ni muhimu kwa matibabu ya wagonjwa mahututi. 

Wataalamu wa magonjwa na wataalam wa maabara pia wanahamasishwa kushiriki katika mapambano katika nchi za Botswana, Msumbiji na Namibia. WHO imekusanya dola za Marekani milioni 12 kusaidia shughuli muhimu za mwitikio katika nchi, kote kanda ya Afrika kwa muda wa miezi mitatu ijayo. 

Pamoja na yote, WHO inasema viwango vya chanjo barani Afrika, vinasalia kuwa chini. Ni watu milioni 102 tu, au asilimia 7.5 ya idadi ya watu wamechanjwa kikamilifu. Zaidi ya asilimia 80 ya watu bado wanahitaji kupokea dozi ya kwanza.