Asante polisi wa UN sasa matukio ya uporaji Kaga-Bandoro yametoweka

Kamishna wa Polisi ajiunga na doria ya kwanza ya MINUSCA huko Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
UN Photo/Catianne Tijerina (Maktaba)
Kamishna wa Polisi ajiunga na doria ya kwanza ya MINUSCA huko Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Asante polisi wa UN sasa matukio ya uporaji Kaga-Bandoro yametoweka

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, polisi wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MINUSCA wameendelea kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya nchi hiyo ili hatimaye wananchi waweze kuendelea na shughuli zao bila bughudha yoyote.

Shughuli za ulinzi wa raia ni pamoja na doria zinazofanywa kwa magari halikadhalika kwa miguu kati ya polisi wa Umoja wa Mataifa na vikosi vya usalama vya CAR. 

Doria ya leo ni katika mji wa Kaga-Bandoro na inafanyika kwa mujibu wa azimio namba 2506 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na lengo ni kuwezesha usafirishaji wa watu na bidhaa bila vikwazo vyovyote. 
Polisi hao kwa pamoja wanafika hadi kwenye masoko ambako wananchi wanaendelea na biashara zao. 

Cecil Coulibaly, ambaye ni Mkuu wa Polisi wa Umoja wa Mataifa eneo la Kaga Bandoro anasema “Kwa ushirikiano na vikosi vya jeshi la polisi tunafanya kazi kwa pamoja. Awali polisi wa CAR hawakuweze kufanya doria eneo lote lakini hivi sasa tunafanya doria pamoja  na tunaweza kuwafikia wananchi na kuwadhihirishia uwezo wa jeshi lao na pia kutaka wananchi nao wawe na ushirikiano na jeshi la polisi, FSI.” 

Ali Abakar, mmoja wa wakazi wa Kaga-Bandoro ni shuhuda wa manufaa ya doria hizo za pamoja akisema “Mambo mengi yamebadilika, kwani zamani doria zilikuwa hazifanyiki katika kitongoji chetu cha 4. Sasa imefanyika kwa miezi mitatu sasa na matukio ya uporaji yametoweka.” 

Ni kwa mantiki hiyo Ali ombi lake ni kwamba doria hizo za pamoja na polisi wa Umoja wa Mataifa na vikosi vya usalama CAR ziendelee.