Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AU yatoa masharti 6 kwa wanaotoa msaada wa chanjo za COVID-19 Afrika

Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.
UNICEF/Daniel Msirikale
Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.

AU yatoa masharti 6 kwa wanaotoa msaada wa chanjo za COVID-19 Afrika

Afya

Kuanzia Januari mosi mwaka 2022 kama kuna nchi au shirika la kimataifa linataka kutoa msaada wa chanjo za Corona au COVID-19 barani Afrika, basi linapaswa kufuata masharti kadhaa yaliyotolewa leo na Muungano wa Afrika AU kwa kushirikiana na mashirika mengine tanzu kama vile kituo cha Afrika cha kudhibiti magonjwa CDC na GAVI COVAX  na AVAT yenye jukumu kuu la uwakala  mkuu wa ununuzi kwa niaba ya AU.

Taarifa ya pamoja kutoka makao makuu ya Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia inasema mpaka sasa Afrika imepokea msaada wa zaidi ya dozi milioni 90, lakini chanjo hizo nyingi zimekuwa zikiletwa kwa mfumo wa dharura huku zikiwa na muda mfupi wa kuweza kutumika hali inayozifanya nchi nyingi zinazopokea kushindwa kujipanga sawasawa kuzitoa kwa wananachi wake kwa usawa na ufanisi. 

Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.
UNICEF/Daniel Msirikale
Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.

Masharti 6 yaliyowekwa na AU 

Jumla ya masharti 6 yametolewa kwa nchi na jumuiya za kimataifa zinazotaka kutoa chanjo , ambayo ni 

1. Taarifa itolewe mapema: 

Nchi zinazopokea chanjo za msaada zinapaswa kutaarifiwa upatikanaji wa chanjo si chini ya wiki 4 kabla ya kuwasili kwake nchini 

2. Kiasi na kutabirika: 

Nchi wafadhili zimetaarifiwa kuwa zinapaswa kujitahidi kutoa dozi kwa wingi na kwa njia inayotabirika, ili kupunguza gharama za ununuzi. Kwa njia hii itasaidia kuratibu shughuli zinazofanywa na AVAT na COVAX za kununua na kusambaza chanjo kwa ajili ya nchi za Afrika. 

3. Kuweka alama: 

Dozi zinazotolewa msaada kwa sasa zimekuwa zikiwekwa alama za kutoka nchi gani kwenda nchi gani, lakini AVAT inapenda zisiwekwe alama hiyo ili kuwezesha usambazaji wa usawa barani Afrika kulingana na uwezo wa nchi kusambaza kwa wananchi wake. 

AU inaonya kwamba kuendelea kutoa chanjo nyingi kwa nchi bila kuangalia uwezo wao wa kuhifadhi katika baridi ili zisiharibike pia kwa kuangalia muda mfupi wake kabla ya kuharibika kunaweza kusababisha chanjo hizo zisiwe na manufaa katika nchi zinapopelekwa ilikinganishwa na iwapo AVAT wangezigawa kwa nchi ambazo zingezitumia ndani ya muda mfupi. 

4. Viambatanisho: 

Michango mingi hadi sasa haijumuishi vifaa muhimu vya chanjo kama vile mabomba ya sindano wala dawa ya kuchanganyia, wala haitoi gharama za usafirishaji hii ikimaanisha kuwa ni lazima nchi zitenge fedha za kuwezesha vitu hivyo, hizi ni gharama za ziada. 
  
Chanjo za msaada zinapaswa kuambatana na viambatanisho vyote muhimu ili kuhakikisha ugawaji na matumizi ya haraka. 

5. Muda mrefu kabla hazijaharibika : 

Chanjo zote za msaada zinazotolewa Afrika wakati zinapowasili zinapaswa kuwa na muda usiopungua wiki 10 kabla  ya muda wake wa kutumika haujamalizika, tofauti na hapo nchi zinazopokea chanjo hizo zinatakiwa kuonesha nia na uwezo wa kuzitumia ndani ya muda mfupi kabla hazijaharibika. 

6. Uharaka wa kutoa majibu: 

Wadau wote wanapaswa kuhakikisha wanatoa majibu ya haraka kuhusu taarifa muhimu. Hii ni pamoja na maelezo muhimu ya usambazaji kutoka kwa watengenezaji (jumla ya kiasi cha chanjo za msaada kinachopatikana, muda wa kuhifadhi, tovuti ya utengenezaji), uthibitisho wa toleo la mchango kutoka kwa wahisani, na kukubalika au kukataliwa kwa mgao kutoka kwa nchi. 
  
Utoaji taarifa za dakika za mwisho zinaweza kutatiza michakato zaidi, kuongeza gharama za ununuzi, kupunguza muda wa chanjo kufaa kutumika na kuongeza hatari ya kuharibika. 
  
Taarifa hiyo pia imesema AVAT, Africa CDC na COVAX zinaendelea kushirikiana na nchi wahisani, watengenezaji chanjo pamoja na washirika katika kuhakikisha viwango masharti haya yanazingatiwa wakati wakiendelea kufanya kazi pamoja ili kufikia malengo ya kuwa na chanjo ya Afrika.