Kumezuka aina mpya ya COVID-19, tahadhari ichukuliwe:WHO

Kituo cha serikali cha kupima COVID-19 huko Johannesburg, Afrika Kusini. (Makataba)
IMF Photo/James Oatway
Kituo cha serikali cha kupima COVID-19 huko Johannesburg, Afrika Kusini. (Makataba)

Kumezuka aina mpya ya COVID-19, tahadhari ichukuliwe:WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limezitaka nchi zote kuzingatia mbinu za kisayansi na za dharura pindi zinapotaka kupiga marufuku safari katika maeneo yanayohusishwa na aina mpya ya virusi vya Corona au COVID-19 iliyobainiwa nchini Afrika Kusini na Botswana. 

Hatua hiyo iliyotangazwa leo Ijumaa imekuja wakati jopo la WHO likijiandaa kukutana ili kutathmini athari zinazowezekana kuletwa na aina hii mpya ya virusi vya Corona iliyopatiwa jina B 1.1.529

Kulingana na mkuu wa masuala ya kiufundi wa COVID-19 kwenye WHO, Dkt. Maria Van Kerkhove, taarifa bado ni chache kuhusiana na aina hiyo mpya ya COVID-19 ambapo aina ya virusi hivyo ina mabadiliko tofauti tofauti hali ambayo inaweza kuleta changamoto katika matibabu iwapo mgonjwa atapata virusi hivyo.

Dkt. Van Kerkhove ameeleza kuwa watafiti kwa sasa wanajaribu kubainisha mabadiliko hayo yalipo na yanaweza kumaanisha nini kwa uchunguzi, matibabu na chanjo. 

Ameongeza kuwa "Itachukua wiki chache kwetu kuelewa ni athari gani lahaja hii inaweza kuleta, kuna kazi nyingi ambayo inaendelea kufanyika kwa sasa. Ni lahaja ambayo iko chini ya ufuatiliaji. Kikundi cha ushauri wa kiufundi cha WHO kitajadili ikiwa itakuwa aina ya kawaida auaina itakayosababisha wasiwasi na endapo ni hivyo, tutaipa jina la Kigiriki, lakini ni jambo la kufuatilia”. 

Mtoa huduma wa kujitolea anayeitwa Trinity anafanya kazi katika hospitali ya COVID-19 huko Nasrec, Johannesburg.
IMF/James Oatway
Mtoa huduma wa kujitolea anayeitwa Trinity anafanya kazi katika hospitali ya COVID-19 huko Nasrec, Johannesburg.

Usibague 

Wataalam hao wa WHO wamewashukuru watafiti kutoka Afrika Kusini na Botswana kwa kushirikisha kwa njia ya uwazi WHO taarifa za aina hiyo mpya ya virusi.

"Kila mtu huko nje usibague nchi ambazo zinashiriki matokeo yao kwa uwazi", limehimiza shirika la WHO, kwani nchi kama vile Uingereza, Ufaransa na Israeli zimefikia hatua ya kufuta safari za ndege za moja kwa moja kutoka Afrika Kusini na mataifa jirani. 

Kulingana na mamlaka ya afya ya Afrika Kusini hadi sasa, wagonjwa walioripotiwa kuwa na aina hiyo mpya ni chini ya 100 ambao wamethibitishwa, hasa miongoni mwa vijana ambao wana kiwango cha chini zaidi cha chanjo nchini humo. 

"Nchi zinaweza kufanya mengi katika suala la ufuatiliaji na mpangilio na kufanya kazi pamoja na nchi zilizoathiriwa au kimataifa na kisayansi kupambana na lahaja hii mpya na kuelewa zaidi kuihusu ili tujue jinsi ya kufanya. Kwa hivyo katika hatua hii WHO imetahadharisha juu ya kutekeleza hatua za kufuta safari.” msemaji wa WHO Christian Lindmeier amewaambia waandishi wa Habari hii leo mjini Geneva Uswis. 

Usafiri wa ndege kati ya Marekani na Uingereza umepungua kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19.
UN News/Daniel Dickinson
Usafiri wa ndege kati ya Marekani na Uingereza umepungua kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19.

Jilinde na uwalinde wengine 

Maafisa wa WHO wamekumbusha ushauri wa hapo awali kwamba watu wanaweza kufanya mengi kujilinda na COVID-19, pamoja na kuendelea kuvaa barakoa na kuzuia mikusanyiko yenye umati wa watu. 

"Kila mtu aliyeko nje anahitaji kuelewa kwamba kadiri virusi hivi vinavyozunguka ndivyo kunavyokuwa na fursa zaidi ya virusi kuweza kubadilika, na ndivyo tutakavyoshuhudia aina zaidi zikijitokeza", amesema Dk. Van Kerkhove. 

Amesisitiza kuwa "Pata chanjo unapoweza, hakikisha unapokea kipimo kamili cha dozi zako na hakikisha unachukua hatua za kupunguza uwezekano wako wa kuambukizwa na ukiwa navyo kujizuia kusambaza virusi hivyo kwa mtu mwingine".