Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa mazao ya chakula iimarishwe- FAO

Mifumo ya uzalishaji chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.
© FAO/Petterik Wiggers
Mifumo ya uzalishaji chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.

Mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa mazao ya chakula iimarishwe- FAO

Masuala ya UM

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya chakula na kilimo duniani SOFA2021, imezitaka nchi duniani kuhakikisha mifumo yao ya kilimo cha mazao ya chakula ina uwezo wa kuhimili changamoto zozote zinazoweza kutokea kama vile janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, ambalo limesababisha ongezeko la njaa duniani.
 

Ikitolewa hii leo huko Roma nchini Italia na shirika la  Umoja wa Mataifa la chakula na duniani, FAO, ripoti hiyo imesema bila maandalizi ya kina dhidi ya majanga yasiyotabirika, majanga yanaweza kukwamisha mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula duniani.

“Janga la Corona, limeangazia mnepo na udhaifu wa mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula,” amesema Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa FAO katika tukio la uzinduzi wa ripoti hiyo lililofanyika kwa njia ya mtandao.

FAO inasema hata kabla ya Corona, dunia haikuwa kwenye mwelekeo wa kufikia lengo la kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030. “Wakati kihistoria uzalishaji wa chakula na mifumo ya usambazaji wa chakula imekuwa hatarini kutokana na hali mbaya za tabianchi, mizozo na ongezeko la bei ya chakula duniani, matokeo ya mara kwa mara ya majanga hayo yanazidi kuongezeka na madhara ni makubwa zaidi.”

Christine Banlog akichagua viazi kwenye soko la jumla la mjini Douala nchini Cameroon.
UN Women/Ryan Brown
Christine Banlog akichagua viazi kwenye soko la jumla la mjini Douala nchini Cameroon.

Janga la Corona lilikwamisha usafirishaji wa vyakula, wakulima walishindwa kuendelea na shughuli za kilimo, maduka ya kuuza vyakula nayo kwingineko yalishindwa kutoa huduma na hivyo kuathiri huduma za lishe.

Ni kwa mantiki hiyo ripoti hiyo iliyopatiwa jina Kuwezesha mifumo cha chakula kuwa na mnepo dhidi ya majanga”  imetathmini uwezo wa mifumo ya kitaifa ya kilimo na chakula na uwezo wa kukabiliana na majanga na inapatia serikali miongozo ya jinsi ya kuimarisha uwezo wa mifumo hiyo kuendana na mazingira bila mkwamo wa kitendaji.

Serikali zifanye nini?

Serikali zinatakiwa kupanua wigo wa vyanzo vya vyakula, uzalishaji, masoko na usambazaji kwa kusaidia pia kampuni ndogo na za kati zinazozalisha vyakula na vyama vya ushirika.

Halikadhalika kuunganisha mtandao wa usafirishaji ili kuepusha mvurugano pindi janga linatokea.
Hatua nyingine ni kujengea uwezo kaya zilizo hatarini ili zisikumbwe na njaa hata janga likitokea kwa kuzipatia njia mbadala za kujipatia kipato na mifumo ya hifadhi ya jamii.

Hii leo takribani kuna watu bilioni 3 wasio na uwezo wa kupata lishe bora ambapo SOFA inakadiria kuwa watu wengine bilioni 1 wataongezeka iwapo vipato vyao vitapungua kwa theluthi moja.

Pakua ripoti nzima ya SOFA2021 hapa.