Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatujawahi kuona mafuriko kama  haya Sudan- Mkazi White Nile

Taswira kutoka juu ya mafuriko katika kambi ya wakimbizi ya Alganaa kwenye jimbo la White Nile nchini Sudan.
UNHCR Video
Taswira kutoka juu ya mafuriko katika kambi ya wakimbizi ya Alganaa kwenye jimbo la White Nile nchini Sudan.

Hatujawahi kuona mafuriko kama  haya Sudan- Mkazi White Nile

Msaada wa Kibinadamu

Tumeishi hapa tangu miaka ya 1950 na katu hatujawahi kushuhudia mafuriko kama haya, amesema mkazi wa jimbo la White Nile nchini Sudan ambako mafuriko makubwa yamesababisha wakimbizi wa ndani kusaka hifadhi kwa wenyeji wao huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wakiendelea kusambaza misaada ya kibinadamu. John Kibego na maelezo zaidi.
 

Kukurukakara za wakimbizi wa kambi ya Alganaa jimboni White Nile nchini Sudan za kupokea misaada kama vile mablanketi, vyakula na madumu ya kubebea maji.

Wakimbizi hawa wanawake, wanaume na watoto wamejikuta hawana makazi baada ya mafuriko kuzingira makazi yao na kuathiri watu 80,000 wakiwemo wakimbizi 30,000.

Sasa wanaishi kwa wenyeji ambao nao hawajui la kufanya kwa kuwa hawajashuhudia mafuriko kama haya yaliyotokana na mvua kubwa katika jimbo la Upper nile nchini Sudan Kusini.
Yahia Ahmed, ni mmoja wa wenyeji ambaye anapatia hifadhi wakimbizi wa ndani ambaye anasema, “Tumekuwa tunaishi eneo hili tangu miaka ya 1950 na tunachoona hivi sasa si hali ya kawaida. Mara chache tumekuwa tukipata mafuriko ya ghafla lakini si kama hivi. Hii ni mara ya kwanza hii inatokea.”
 

Mafuriko haya yamekumba kambi ya wakimbizi ya Alganaa miezi michache tu tangu ianzishwe na sasa imetwama na kimbilio la wakimbizi ni katika kambi zingine sambamba na kwa wenyeji ambao nao hawana kinyongo.

Sunday Rock, naye ni mkimbizi kutoka Sudan Kusini lakini amekubali kuhifadhi wakimbizi wenzake akisema, “Tunajivunia kwamba wakimbizi wa ndani walipofika, tulikubaliana kuwasaidia kwa sababu sote ni ndugu na tumetoka nchi moja. Tunatumia pamoja chochote kile tulichonacho.”

UNHCR inasema msaada zaidi unahitajika ili kuweza kusaidia wakimbizi hao waliofurushwa kutoka kambini kutokana na mafuriko.