Mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi waleta mabadiliko chanya-UNHCR 

Wakimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Kyangwali wafanya mjadala kuhusu afya ya uzazi.
UN News/ John Kibego
Wakimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Kyangwali wafanya mjadala kuhusu afya ya uzazi.

Mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi waleta mabadiliko chanya-UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR inaonesha kuwa jamii ya kimataifa imeitikia vema wito wa kuwajibika pamoja katika kusaidia wakimbizi kupitia mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, GCR.

Ikitolewa leo jijini Geneva, Uswisi, ripoti hiyo ikihusisha kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 inaonesha maendeleo chanya kwenye usaidizi kwa nchi za kipato cha chini zinazohifadhi wakimbizi sambamba na wakimbizi kuweza kupata elimu na ajira licha ya kwamba hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa.

Kamishna Msaidizi wa UNHCR anayehusika na hifadhi ya wakimbizi Gillian Trigss anasema ingawa hivyo taswira ni mchanganyiko, “tunaona nchi zenye uwezo mdogo zikiendelea kubeba mzigo mkubwa kwa wakimbizi kutoka mizozo mipya na ile iliyodumu muda mrefu. Wakati huo huo tunashuhudia viashiria vizuri kutoka serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na benki za maendeleo zikisaidia kujaribu kuziba pengo lililoko.”

Wakimbizi wa ndani wamepatiwa mafunzo ya kuwaandaa samaki kwa ajili ya kwenda kuwauza
© FAO Cameroon
Wakimbizi wa ndani wamepatiwa mafunzo ya kuwaandaa samaki kwa ajili ya kwenda kuwauza

Ripoti inaonesha ingawa fedha zaidi zinahitajika kufanikisha, kumekuwepo na usaidizi wa kimaendeleo kupitia makubaliano kati ya nchi mbili na tangu mwaka 2016 fedha zimepelekwa kwa nchi za kipato cha chini zinazohifadhi wakimbizi.

Benki za maendeleo nazo zimejitoa kimasomaso kuchukua hatua dhidi ya janga la wakimbizi kwa kutoa jumla ya dola bilioni 2.33.

Ripoti pia inaonesha kuwa wakimbizi wengi zaidi walipata suluhu kati yam waka 2016 na 2021 ikilinganishwa na miaka mitano iliyotangulia, bado mizozo inayoendelea inazuia wakimbizi kurejea nyumbani.
“Ikiwa wakimbizi 9 kati ya 10 wanahifadhiwa katika nchi zinazoendelea na na janga la Corona au COVID-19 limeleta athari mbaya, suala la kugawana majukumu ambalo ni msingi wa mkataba wa wakimbizi linapaswa kuimarika zaidi ili kukabili changamoto za sasa,” amesema Triggs.

Bofya hapa kupata ripoti nzima.