Mashirika 5 ya UN yaunga mkono ushirika wa kuhakikisha kila mtoto anapata mlo shuleni 

16 Novemba 2021

Kwa wanufaika wa mpango wa mlo shuleni watafurahia sana kusikia taarifa hii iliyotolewa leo na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata mlo bora shuleni ifikapo mwaka 2030.

Mashirika hayo yanaunga mkono ubia wa kimataifa wenye lengo la kuimarisha haraka lishe bora, afya na elimu kwa watoto wote ulimwenguni wenye umri wa kwenda shule baada ya shule kufungwa kutokana na janga la Corona au COVID-19.

Taarifa ya pamoja ya mashirka hayo lile la mpango wa chakula duniani, WFP, kuhudumia watoto, UNICEF, elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, chakula na kilimo FAO pamoja na lile la afya WHO ambayo imetolewa leo jijini New York Marekani imesema mwaka 2020 janga la COVID-19 lilisababisha shule kufunguwa na mamilioni ya watoto duniani kote hawakunufaika na mpango wa mlo shuleni na huduma nyingine kama vile utoaji wa dawa za minyoo, chanjo na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.

Watoto wakipata mlo shuleni nchini Msumbiji
© UNICEF/UN051605/Rich
Watoto wakipata mlo shuleni nchini Msumbiji

Zaidi ya watoto milioni 150 bado wanakosa mlo shuleni na huduma hizo kwa hiyo mashirika hayo yametoa azimio la pamoja la kusaidia ubia wa mlo shuleni unaotekelezwa katika nchi zaidi ya 60 na ukiongozwa na Ufaransa na Finland ambazo dira yao ni kuona kila mtoto mwenye mahitaji anapata furrsa ya kupata mlo bora shulen iifikapo mwaka 2030.

MAshirika hayo yamesema mipango ya milo shuleni hainufaishi watoto pekee bali pia ni chanzo cha mabadiliko kwenye mifumo ya chakula kwa kuwezesha kula vyakula vinavyolimwa kwenye eneo lao na kujenga fursa za wakulima wadogo kujipatia kipato.

Kupitia azimio hilo kila shirika litachangia utaalamu wake kwenye ubia huo.

Akizungumzia mpango wao, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley amesema “ubia wa mlo shuleni una uwezo wa kusaidia nchi kuibuka kutoka janga la COVID-19, kurejesha watoto shuleni, kurekebisha athari za janga kwenye elimu yao, kufungua fursa za ajira kwenye eneo husika na kuwezesha wakulima wadogo kuwa na kipato endelevu, na tunajivunia kuunga mkono ubia huu.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter