Pfizer yaridhia dawa yake ya kutibu COVID-19 izalishwe kwa gharama nafuu

16 Novemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa za tiba kwa gharama nafuu, UNITAID, leo limetangaza makubaliano ya kuwezesha dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona, COVID-19 kutoka kampuni ya Pfizer ipatikane kwa gharama nafuu kwa nchi za kipato cha chini na kati. 

Msemaji wa UNITAID Hervé Verhoosel ametangaza hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari akisema makubaliano hayo ya hiari ni kupitia mpango wa kurahisisha upatikanaji wa hataza za dawa au MPP ulioanzishwa na shirika hilo ili nchi za kipato cha chini na kati ziweze kumudu dawa za kuokoa maisha.

Dawa hiyo PF-07321332 ambayo bado iko kwenye mchakato wa kuidhinishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO inatumika kwa kuchanganywa pamoja na dozi kidogo ya dawa aina ya Ritonavir.

“Makubaliano ya leo yanaamanisha kuwa MPP itawezesha uzalishaji wa nyongeza na usambazaji wa dawa hiyo, ambapo kampuni zenye sifa za kutengeneza dawa kwa gharama nafuu zitapatiwa leseni ya kufanya hivyo ili zipatikane kwa wingi,” amesema Verhoosel.

Kampuni husika zitatengeneza dawa hiyo kwa ajili ya nchi 95 zikiwemo za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na hivyo kufikia asilimia 53 ya wakazi wa dunia.

Pfizer haitopokea mrahaba za mauzo ya dawa hizo kwa nchi za kipato cha chini na pia itaondoa malipo hayo kwa mauzo ya dawa hizo kwa nchi zilizotajwa kwenye makubaliano hayo kwa kipindi chote ambacho COVID-19 itasalia kuwa janga la afya kwa umma duniani.

Bwana Verhoosel amesema hii ni mara ya kwanza kwa dawa hii kupatiwa leseni ya kuzalishwa kwa gharama nafuu na ni hatua muhimu kusaidia kuhakikisha kuwa mbinu mpya za kukabili COVID-19 zinapatikana nchi za kipato cha chini na kati kwa wakati ule ule ambapo dawa hizo zinapatikana katika nchi tajiri.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter