Mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zaleta mapigano nchini Cameroon

Watu huyakimbia makazi yao mara kwa mara kaskazini-mashariki mwa Cameroon kutokana na migogoro.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Watu huyakimbia makazi yao mara kwa mara kaskazini-mashariki mwa Cameroon kutokana na migogoro.

Mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zaleta mapigano nchini Cameroon

Tabianchi na mazingira

Wakati Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi COP26 ukiwa umemalizika mwishoni mwa wiki huko Scotland huku Afrika ikisema haijafanikiwa ilivyotarajia, huko nchini Cameroon mabadiliko ya tabianchi yameleta uhasama baina ya wafugaji, wakulima na wavuvi, sababu kubwa ya ugomvi huo ni mbinu walizobuni za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mvua ni chache sana. Sijui sababu ya mabadiliko ya tabianchi lakini inabidi tubadilike na kuwahifadhi samaki wakati wa kiangazi. Mavuno tunayapata kwenye kilimo hayatoshi.” ndio asemavyo Assiam Yere, mkimbizi wa ndani eneo la Musgum nchini Cameroon.

Katika kutafuta suluhu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakulima na wavuvi wa Musgum wakaona ni vyema kuchimba mashimo makubwa kwa ajili ya kuhifadhi maji ya mvua ili yawasaidie kipindi cha ukame.

Lakini wafugaji waarabu wa Choa hawataki kuyaona wala kuyasikia sababu kwao ni mitego ya kifo kwa ng'ombe wao kwani huteleza kwenye miteremko mikali, huvunja miguu na wakati mwingine kuzama kabisa katika mashimo hayo.

Robert Mati ni mkulima wa kijiji cha Missiska akisimulia mapigano yaliyotokea mwezi Agosti mwaka huu kati ya wafugaji na wavuvi yalisababisha vifo vya watu 45 na majeruhi 74. Vijiji 19 viliteketezwa kwa moto na zaidi ya watu 23,000 walilazimika kuyakimbia makazi yao amesema

“Waarabu wa Choa walikuja kufukia mashimo tuliyochimba. Kwa kweli, walitaka tuyajaze mchanga mashimo siku hiyo hiyo. Ikiwa hatukufanya hivyo walisema wangetuua”

Naye mwanakijiji wa kijiji cha  Demza Issa Mahmat, anasema "Kwa sasa, kila mtu anaogopa, usiku ukiwa kitandani, hakuna kulala, wengine wanalala nje."

Wanawake wanapanda miti katika ardhi iliyoharibiwa katika pwani ya Ikweta ya Cameroon.
CIFOR/Ollivier Girard
Wanawake wanapanda miti katika ardhi iliyoharibiwa katika pwani ya Ikweta ya Cameroon.

Hofu hii ndio imesababisha maelfu kuyakimbia makazi yao, kuvuka mto Logone hadi nchini Chad. Na ndani ya miezi miwili, takriban watu 8,800 wamesajiliwa kuwa wakimbizi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhdumia wakimbizi - UNHCR.

Juhudi za UNHCR zimewezesha zaidi wakimbizi wa ndani 12,000 kurejea makwao ingawa wengi wao wanasema hawalali fofofo.

Kwa mujibu wa UNHCR mabadiliko ya tabianchi yamekuwa chanzo kikuu cha watu kuyahama makazi yao na sababu kuu inayowazuia watu kurudi. Wakimbizi wengi wanasema watakabiliwa na njaa ikiwa watarudi nyumbani.