Hongera UNESCO kwa kutimiza miaka 75: Guterres

12 Novemba 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelipongeza shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, kwa kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. 

Kupitia ujumbe wake wa video kwa maadhimisho hayo Antonio Guterres amesema shirika la UNESCO lilianzishwa kama nguzo ya mfumo wa Umoja wa Mataifa baada ya kufunguwa ukurasa wa giza nene katika historia ya binadamu ambao ni vita vya pili vya dunia.

Ameongeza kuwa "Kwa miaka 75, UNESCO imekuwa ikichagiza majadiliano na maelewano. Na vitu kama maeneo ya urithi wa dunia, maeneo ya hifadhi ya kimataifa na kituo cha utafiti cha CERN, vyote hivyo vimeibuka kwa sababu ya UNESCO” .

Katibu mkuu amesisitiza kuwa katika wakati kama huu wa “pengo kubwa la usawa, migogoro ya kimazingira, mivutano ya kiasa na majanga kama COVID-19, jukumu la UNESCO ni muhimu zaidfi kuliko wakati mwingine wowote.” 

Kurejesha imani na mshikamano 

Gutetterres amesema na jukumu hilo ni katika kurejesha Imani na mshikamano, katika kuhakikisha fursa za elimu kwa wote, kuchagiza tamaduni tofauti na kusongesha mchakato wa teknolojia kwa faida ya wote. 

UNESCO ambayo inashirikiana na wadau mbalimbali katika kazi zake inaanzisha mkataba mpya wa kijamii wa ajili ya elimu na mafunzo ya muda mrefu.

Pia inaandaa nyenzo mpya za kukabiliana na kauli za chuki na habari potofu. Mbali ya hayo Guterres amesema inazindua mipango mkakati kwa ajili ya nchi ya Iraq na Lebanon, kwa lengo la kutumia elimu na urithi kuponya na kujenga upya kwa mataifa hayo. 

Katibu mkuu wamesisitiza kwamba “kila moja ya juhudi hizi inadhihirisha umuhimu wa UNESCO kuwa katikati ya mtandao wa kimataifa, ulio jumuishi na wenye ufanisi zaidi ambao hunaleta manufaa yanayoonekana kwa watu duniani kote."

Shirika la UNESCO lilianzishwa rasmi tarehe 16 Novemba mwaka 1945.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter